Hii ni kwa mujibu wa shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch na lile la kutetea haki za wanawake nchini Kongo la SOFEPADI, unyanyasaji huo umekuwa ukifanywa na wanachama wa makundi matano yenye silaha yasiyo ya kiserikali na jeshi la Kongo huko mashariki mwa Kongo.

Matukio hayo yameripotiwa zaidi katika majimbo ya Ituri,Kivu Kaskazini na Kivu Kusini ambapo imeelezwa kupunguzwa kwa ufadhili na ufikiwaji mdogo wa huduma za afya kumeliathiri zaidi kundi la wanawake na wasichana kutokana na kliniki nyingi zinazotoa huduma za afya na usadizi mwingi kulazimika kufungwa kutokana na kuyumba kwa hali ya usalama katika maeneo hayo.

Kwa mujibu wa mkurugenzi wa migogoro wa shirika la human rights watch Ida Sawyer, makundi yenye silaha na vikosi vya kijeshi wamekuwa wakitumia unyanyasaji wa kijinsia kama moja ya silaha ya kivita mashariki ya Kongo huku manusura wa uhalifu wakikutana na vikwazo vya kutokujali na kudumaa kwa mfumo wa huduma za afya.

DR Kongo Mugunga 2013 | Wanawake katika kambi za watu waliokimbia makazi yao
Agosti 22, 2013: Wanawake watatu ambao wamefunzwa kutengeneza matofali kwa kutumia vumbi la mbao, karatasi na maji katika kambi ya Mugunga III ya watu waliokimbia makazi yao, magharibi mwa Goma, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Mmoja wao alibakwa na sasa anaogopa sana kwenda kukusanya kuni katika Hifadhi ya Virunga.Picha: Habibou Bangre/AFP/Getty Images

Kundi la waasi la M23 na wanajeshi wa Allied Democratic Forces (ADF) linalofandhiliwa na dola la kiislamu (islamic state) yametuhumiwa kufanya unyanyasaji kwa wanawake na wasichana kwa muda mrefu kwenye makambi huko Kivu ya Kaskazini.

Shirika la umoja wa mataifa la idadi ya watu (UNFPA) liliripoti zaidi ya visa elfu themanini (80,000) vya ubakaji mashariki mwa Kongo kati ya Januari na Septemba 2025 ikiwa ni ongezeko la asilimia 32 kutoka kipindi kama hicho kwa mwaka 2024.

Baadhi ya waathirika waambukizwa Virusi vya Ukimwi

Baadhi ya waathirika wa mapigano hayo wameripotiwa kupata maambukizi ya virusi vya Ukimwi na  wengine wakipata ujauzito baada ya kufanyiwa vitendo vya ubakaji huku uamuzi wa Marekani kupunguza ufadhili wake kwenye sekta ya afya kukitajwa kuchangia kusinyaa kwa huduma za afya katika maeneo hayo ya mapigano.

Hospitali ya Panzi huko Bukavu, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
Daktari amesimama katika chumba ambacho kundi la wanawake wa Kongo, waathiriwa wa ubakaji, wanasubiri matibabu 07 Novemba 2003 katika moja ya wodi za Hospitali ya Panzi ya Bukavu, katika mji mkuu wa Kivu kusini mwa Bukavu, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).Picha: Gianluigi Guercia/AFP/Getty Images

Licha ya kutoa msamaha kwa programu za kuzuia maambukizi ya Virusi vya Ukiwmi (VVU) ikiwemo utoaji wa  vifaa vya PEP, serikali ya Marekani ilisitisha ghafla ufadhili huko mashariki mwa Kongo huku wito ukitolewa kwa  Serikali ya Marekani  kurejesha ufadhili huo kwa haraka ili kunusuru hali mbaya inayoendelea mashariki mwa Kongo.

Mratibu wa kitaifa  SOPEFADI Sandrine Lusamb amesema Kongo inapaswa kuendeleza juhudi zake za kukomesha unyanyasaji wa kijinsia na kutekeleza mpango wake wa mpito wa haki kwa kushirikiana na umoja wa mataifa ili kuhakikisha waathirika wote wanapata haki zao.

Serikali ya Kongo tayari imeanza programu maalum ya kutoa fidia kwa waathirika wa unyanyasaji wa kijinsia na uhalifu mwingine mkubwa pamoja na msaada wa dharura kwa wale ambao wamenusurika na unyanyasaji wa kijinsia ambapo mpaka sasa waathirika takriban 1,000 katika majimbo ya Ituri,Kasais na Bas Congo wamedaiwa kulipwa fidia zao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *