
Kocha wa Morocco Walid Regragui amepinga vikali madai kwamba timu yake inanufaika na maamuzi ya upendeleo ya waamuzi kama mwenyeji wa michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika AFCON.
“Sisi ndiyo timu ambayo kila mtu anataka kuifunga. Kutokana na hali hiyo, watu watatafuta kila aina ya sababu kudai kwamba Morocco inapendelewa,” alisema Regragui baada ya ushindi wa 2–0 dhidi ya Cameroon katika robo fainali.
“Faida pekee ambayo Morocco inayo kwenye AFCON ni kucheza mbele ya mashabiki 65,000. Kilichobaki ni matukio ya uwanjani—sisi tunazungumza uwanjani.”
Kauli ya Regeagui ameitoa baada ya Cameroon kuonekana kunyimwa penalti mbili ambazo wachambuzi wengi wamezitaja kuwa wazi, hali iliyomfanya mwamuzi Dahane Beida kuonekana kuipendelea timu ya nyumbani.
Beki wa Morocco Adam Masina alihusika katika matukio yote mawili. Awali, alionekana kumgusa Bryan Mbuemo kwenye mguu wa kulia baada ya kuukosa mpira ndani ya kisanduku wakati Cameroon wakitafuta bao la kusawazisha. Baadaye, katika dakika za mwisho, alionekana kumchezea vibaya Etta Eyong ndani ya eneo la penalti.
Beida, ambaye pia alichezesha fainali ya michuano iliopita, aliamua pia kutompa Bilal El Khannouss kadi ya pili ya njano baada ya kumzuia Danny Namaso kwenye shambulizi la kushtukiza muda mfupi kabla ya Ismael Saibari kufunga bao la pili na la ushindi.
“Watu wengi wanataka kuamini au kuwafanya wengine waamini kwamba tunapata faida kutoka kwa waamuzi. Mimi binafsi nimeona penalti ambazo zingeweza kutolewa kwa upande wetu. Kuhusu waamuzi, mimi sijawahi kuzungumzia kuhusu mwamuzi,” amesisitiza Regragui.