Shirika la habari la serikali ya Syria, SANA, liliripoti kuwa wapiganaji wa mwisho wa SDF waliondoka eneo hilo kwa basi usiku kucha wakielekea kaskazini-mashariki mwa Syria, eneo linalojitawala la Wakurdi, na kwamba hali ya usalama ilikuwa ikirejea taratibu katika vitongoji viwili vinavyokaliwa zaidi na Wakurdi. SANA pia iliripoti kuwa vikosi vya usalama vya serikali vimewekwa ndani ya Sheikh Maqsoud, ambako vinazima vilipuzi vilivyoachwa nyuma na wapiganaji wa Kikurdi.

Aidha, Naibu Gavana wa Aleppo, Ferhad Khorto, amesema kuwa hakuna mgawanyiko wa kikabila au wa kidini nchini Syria. Akizungumza na Kituo cha Habari cha TRT, Khorto amesema Wasyria wote wanaishi pamoja bila ubaguzi, akiongeza kuwa hakuna mgawanyiko kati ya Wakurdi, Waturuki, Waarabu, Wakristo au Waislamu.

Amesema ”Alhamdulillah, tumefika hapa. Tulishuhudia furaha ya uhuru wa Syria mwaka mmoja uliopita, na leo tunashuhudia furaha ya uhuru wa pili. Tulijaribu kuwaondoa watu kutoka hapa na kuwahamishia sehemu salama. Baadhi yao walichagua kubaki kwenye maeneo salama. Wengine walienda kuishi na ndugu zao, iwe Aleppo, Afrin au maeneo mengine.”

Syria Aleppo 2026 | Raia wakimbia wilaya ya Sheikh Maksoud baada ya makubaliano ya serikali na SDF kuvunjika
Watu wakiondoka eneo la Sheikh Maksoud kufuatia kuvunjika kwa makubaliano kati ya serikali ya Syria na Vikosi vya Kidemokrasia vya Syria (SDF), huko Aleppo, Syria, Januari 10, 2026.Picha: Khalil Ashawi/REUTERS

Utekelezaji dhaifu wa makubaliano wachochea mapigano

Mapigano hayo, yaliyozuka Jumanne wiki iliyopita, yalihusishwa na kusuasua kwa mazungumzo kuhusu kuunganisha taasisi zinazoendeshwa na Wakurdi pamoja na wapiganaji wa SDF katika dola ya Syria, kufuatia makubaliano yaliyofikiwa kati ya pande zote mwezi Machi mwaka jana. Kila upande umeutuhumu mwingine kwa kuchochea mapigano hayo.

Kamanda wa SDF, Mazloum Abdi, alisema katika chapisho kwenye mtandao wa kijamii wa X kwamba makubaliano ya kusitisha mapigano na uokoaji salama wa raia na wapiganaji yalifikiwa kupitia upatanishi wa kimataifa kutoka vitongoji vya Aleppo vya Sheikh Maqsoud na Ashrafiyeh.

Kwa mujibu wa Shirika la Uangalizi wa Haki za Binadamu la Syria linalofuatilia vita, ghasia hizo zimesababisha vifo vya angalau watu 105, wakiwemo raia 45. Mapigano hayo yanachukuliwa kuwa makali zaidi tangu kuondolewa madarakani kwa mtawala wa muda mrefu Bashar al-Assad zaidi ya mwaka mmoja uliopita.

Wakazi wa kitongoji cha Ashrafiyeh, eneo la kwanza kati ya mawili yaliyoangukia mikononi mwa jeshi la Syria, walianza kurejea majumbani mwao kukagua uharibifu, wakikuta vipande vya mawe na vioo vilivyovunjika vimetapakaa mitaani.

Umoja wa Mataifa ulisema unajaribu kupeleka misafara zaidi ya misaada katika vitongoji hivyo ikiwa na chakula, mafuta, blanketi na mahitaji mengine ya dharura.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *