Waziri Mkuu wa India Narendra Modi na Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz wamekutana siku ya Jumatatu katika mji wa Gadhinagar kwenye jimbo la Gujarat lililopo magharibi mwa India. Mkutano wao ulilenga kuuchochea uhusiano wa kiuchumi na usalama kati ya India, taifa la Asia Kusini na Ujerumani nchi yenye Uchumi mkubwa barani Ulaya.
Mkutano huo umefanyika wakati wa ziara rasmi ya kwanza ya Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz nchini India ukisisitiza uzito unaoongezeka wa mkakati wa ushirikiano wa pande nyingi unaozingatia sheria, mazingira ya wazi na ya haki katika biashara na uwekezaji mienendo inaoyungwa mkono na Umoja wa Ulaya.
Ujerumani na India zinalenga kuupanua ushirikiano wao katika sekta ya ulinzi, na wizara za ulinzi za nchi hizo mbili zimetiliana saini kuhusiana na nia hiyo hii leo Jumatatu.
Mbali na sekta ya ulinzi, Ujerumani na India pia zimetia saini makubaliano mengine ya kuimarisha ushirikiano katika sekta za ukuzaji wa ujuzi, afya na elimu, wakati ambapo mataifa hayo mawili yanapojaribu kupunguza utegemezi wao kwa China.
Kwa jumla, matamko 27 ya nia yametiwa saini kuanzia ushirikiano katika uchimbaji wa madini adimu hadi kukuza vipaji vya mchezo wa mpira wa magongo (Hockey) na pia katika swala la kuajiri wafanyakazi wenye ujuzi katika huduma ya afya nchini Ujerumani.
Baada ya mazungumzo hayo ya pande mbili, Waziri wa India Narendra Modi amebainisha kuwa Ujerumani ni mshirika muhimu zaidi wa kibiashara wa India katika Umoja wa Ulaya na amesema yeye na Merz wanatafuta kuukuza zaidi uhusiano wan chi zao.
Ziara ya siku mbili ya Kansela Merz nchini India, ambayo ni ya kwanza tangu aingie madarakani, inafanyika wiki kadhaa kabla ya mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya na India uliopangwa kufanyika mjini New Delhi.
India na Ujerumani zinasherehekea miaka 75 ya uhusiano wa kidiplomasia mwaka huu wa 2026, zikiashiria hatua muhimu katika ushirikiano wao wa muda mrefu ulioanza muda mfupi baada ya Vita vya Pili vya Dunia. India ilikuwa miongoni mwa nchi za mwanzo kuitambua Ujerumani Magharibi mnamo mwaka wa 1951.
Umauzi wa Merz kuifanya India kuwa nchi ya ziara yake ya kwanza barani Asia unahusiana zaidi na mabadiliko na misukosuko ya sasa katika mpangilio wa dunia.