Wanawake wanapozungumzia kuhusu kukoma kwa hedhi au Menopause kama inavyofahamika kitaalamu, na matatizo yanayohusiana nayo, ikiwemo kukosa usingizi, mtu kushindwa kuwa makini, uchovu, kuumwa kipandauso, mabadiliko ya hisia, mara nyingi huzishusha sauti zao na kuwa watu wa kunong’ona.
Kwa sasa kuna wanawake milioni 11 waliofikia umri wa kukoma kwa hedhi nchini Ujerumani, ambao wengi wao wanateseka kutokana na mabadiliko ya homoni, lakini mada hii bado ni mwiko kuzungumziwa.
Zaidi ya wanawake milioni 9 ya wanawake hawa, wako katika nguvu kazi ya taifa. Wanaunda takribani moja ya tano ya idadi ya watu wanaofanya kazi.
Wakati huo huo, theluthi moja ya kampuni za Ujerumani zimeripoti kuhusu uhaba wa wafanyakazi wenye ujuzi. Takwimu hizo ni kulingana na utafiti uliofanywa Machi, 2024 na Taasisi ya Utafiti wa Uchumi ya Ifo. Mabadiliko ya idadi ya watu yanamaanisha kwamba hili linaweza kuwa tatizo zaidi katika siku zijazo.
Ustawi wa wafanyakazi ni muhimu
Hii inafanya kuwa muhimu zaidi kuliko hapo awali kwa waajiri kuangalia na kutunza ustawi wa wafanyakazi wao. Lakini hadi sasa matatizo ya wanawake wanaopitia kipindi cha ukomo wa hedhi, mara nyingi yamekuwa yakipuuzwa.
Karibu theluthi moja ya wanawake hupata dalili kali ambazo zinaweza kudhoofisha uwezo wao wa kufanya kazi.
Mbali na kupata hisia za ghafla za joto kali na jasho usiku, dalili nyingine za kukoma kwa hedhi zinaweza kujumuisha maumivu ya viungo, mapigo ya moyo kupiga kwa kasi sana, usahaulifu, mtu kushindwa kuwa makini, hisia za mfadhaiko, na mtu kupunguza kujithamini.
Kipindi cha kukoma hedhi kwa kawaida huanza wakati mwanamke anapokuwa na umri wa kati ya miaka 40 hadi mwishoni mwa miaka 40, na kwa kawaida kipindi hicho hudumu kati ya miaka 10 na 15.
Ni kipindi cha maisha ambapo mara nyingi watoto huondoka nyumbani, na wanawake wanapaswa kuwa katika nafasi ya kuanza tena kazi. Ukweli ni tofauti kabisa.
Gharama kubwa ya kifedha
Kulingana na Andrea Rumler kutoka Shule ya Uchumi na Sheria ya Berlin, dalili za kukoma hedhi zinaigharimu Ujerumani takribani euro bilioni 9.5 kwa mwaka katika uzalishaji mdogo wa kiuchumi. Kampuni zinapoteza takribani siku milioni 40 za kazi.
Mwaka 2023, Rumler alifanya utafiti kwa zaidi ya wanawake 2,000 wenye umri kato ya miaka 28 na 67. Karibu robo yao walisema dalili za kukoma hedhi zilikuwa sababu ya kupunguza saa zao za kazi, na zilisababisha takribani theluthi moja kubadili kazi zao. Mmoja kati ya 10 alisema kwamba alikusudia kustaafu mapema, au tayari alikuwa amefanya hivyo, kwa sababu ya kukoma hedhi.
Kufanya kati wakati wa kipindi cha kukoma hedhi ni vigumu zaidi katika baadhi ya kazi kuliko nyingine. Kwa mfano, kama afisa wa polisi wa kike aliyeko kwenye doria ghafla anapata hedhi na kutokwa damu nyingi, au tatizo la kibofu cha mkojo, sio mara zote kuna choo cha karibu anachoweza kukifikia.
Dalili za kukoma hedhi ni tatizo hasa kwa wanawake wanaofanya kazi katika sekta ya umma. Walimu, wafanyakazi wa kulea watoto, wauguzi, na wauzaji wa maduka, hawawezi kufanyia kazi nyumbani, au kupumzika wanapohitaji.
Hofu ya unyanyapaa na ubaguzi
Kwa wanawake wengi, kutoweza kuzungumza kwa uwazi kuhusu kukoma hedhi, ni mzigo mkubwa. Zaidi ya nusu ya wanawake katika utafiti wa Rumler walisema kuwa kukoma hedhi ilikuwa nada isiyofaa kuzungumzwa katika sehemu zao za kazi.
“Wanawake wengi walioko katika kipindi hiki cha maisha wanateseka kazini, lakini hawazungumzii kuhusu hilo, kwa kuona aibu, au kutokuwa na uelewa, au kwa hofu ya kunyanyapaliwa,” alifafanua Rumler.
Hii ndiyo sababu kampuni zinahitaji kuwaelimisha watu kuhusu madhara na dalili za ukomo wa hedhi. Taarifa hii ni muhimu sio tu kwa wanawake wanaoathirika, lakini pia kwa wafanyakazi wengine na mameneja.
“Kila mara nasikia kutoka kwa madaktari wa kampuni, au maafisa katika ofisi ya rasilimali watu wanaoshughulikia nada hii kikamilifu, kwamba mabosi wao huipuuza na kusema sio suala muhimu,” alibainisha Rumler.
Mbali na kuuondoa mwisho wa kuijadili nada ya kukoma hedhi, ni muhimu pia ikiwa wanawake watakuwa na uwezo wa kurekebisha saa zao za kazi na utaratibu wao kulingana na mahitaji yao.
Saa za kazi zinazobadilika badilika, ratiba ya kazi inayoendana na mahitaji, na mapumziko ya wakati unaofaa, yanaweza kusaidia kuondoa uchovu, mtu kuwa makini, kutolala, na yanaweza kuimarisha ufanisi na tija kazini kwa kiasi kikubwa.
Uingereza ni mfano wa kuigwa
Katika miaka ya hivi karibuni, mambo yameanza kubadilika. Uingereza imepata maendeleo makubwa.
Bunge la Uingereza lilianzisha mafunzo kuhusu ukomo wa hedhi katika maeneo ya kazi, na kutoa muongozo kuhusu nada hii kama sehemu ya ukaguzi wa kawaida wa afya unaofanywa na Huduma ya Afya ya Serikali, NHS.
Zaidi ya mashirika 7,800 sasa yamesaini mwongozo wa hiari unaojulikana kama Ahadi ya Ukomo wa Hedhi Mahali pa Kazi. Mashirika hayo ni pamoja na kampuni ya simu ya Vodafone, Shirika la Utangazaji la Uingereza, BBC na maduka makubwa ya Tesco.
Ofisi nyingine zilizosaini ni zile za serikali za mitaa, shule, mashirika ya kutoa misaada, watoa huduma za afya, na kampuni ndogo katika sekta nyingi tofauti.
Ukomo wa hedhi bado ni tatizo Ujerumani
Kwa mfano kampuni ya simu ya Vodafone inawasaidia wafanyakazi wake wa kike kupata mafunzo ya mtandaoni kuhusu ukomo wa hedhi, na kwa kutoa saa za kazi zinazobadilika.
Kampuni ya uhasibu ya PwC, imeanzisha mpango wa “Ukomo wa Hedhi ni Muhimu,” kwa kulipia matibabu ya wanawake ili watibiwe matatizo yanayohusiana na ukomo wa hedhi. Aidha, imewapatia App ya afya inayotoa ushauri wa tiba kwa njia ya simu.
Nchini Ujerumani, utafiti kwa waajiri uliofanywa na shirika la the-change.org, mwaka 2024 ulionyesha kuwa asilimia 63 bado wanaona ukomo wa hedhi kama mada “binafsi” au ya “faragha.”
Asilimia 74 ya kampuni zilizohojiwa hazikuwa na hatua zozote za kuwasaidia wanawake wanaopitia kipindi cha kukoma hedhi. Asilimia 7 pekee walisema walitoa msaada mkubwa.
