Kulingana na ripoti hiyo, inakadiriwa kuwa abiria hao watazidi kuongezeka kutokana na uwepo wa safari nyingi za ndege ndani na nje ya nchi.
Ongezeko hilo la abiria linawafanya wabunifu wa masuala ya teknolojia kuumiza kichwa na kutafuta njia za kuwarahisishia abiria namna ya kupata taarifa za usafiri wa anga. Mingoni mwa wataalamu hao ni Emma Alice Kizito mbunifu wa App ya Akili Mnemba inayoitwa SKY AI.
Programu hii imeundwa kwa ajili ya kurahisisha maisha ya watumiaji wa usafiri wa anga. Kwa kawaida katika uwanja wa ndege, kila abiria huwa anafikiria usafiri wake utakaomtoa sehemu moja kwenda nyingine.
Kujua taarifa za safari
Baadhi ya abiria wanaonekana kurundikana kwenye ubao wa matangazo, huku wengine wakiwauliza masuala kadhaa maafisa wanaofanya kazi katika uwanja wa ndege.
Mapinduzi ya Akili Mnemba inampa fursa Emma kutengeneza App ya SKY AI ambayo imekuwa ikirahisisha shughuli za Mamlaka ya Anga Tanzania, TCAA pamoja na mashirika ya ndege ya ndani na nje ya nchi.
Emma anasema mara nyingi kampuni yoyote lazima ifanye kazi kwa kufuata miongozo, lakini kuiandaa huwa inachukua miezi. ”Tuliunda mfumo unaokagua miongozo hiyo yaani Manual Review Adjust Regulations na kubaini kutokuwepo kwa uzingatiaji wa sheria na kukupa maeneo sahihi ya kurekebisha,” alibainisha Emma.
Kulingana na Emma, kupitia App ya SKY AI wamefanikiwa kupunguza kazi za wiki kadhaa kuwa chache na wameongeza pia afya ya anga kwani hapo ndipo usalama unapoanza.
”Tuna suluhisho maalumu kwa ajili ya watumishi wa afya wa anga. Daktari anaingiza vipimo vya rubani na App yetu iliyopewa mafunzo inahakiki matokeo hayo na papo hapo inampa daktari miongozo ya kitaalamu na miongozo ya kisheria ili kufanya maamuzi sahihi kama rubani anafaa kuruka au la!” Alisema mbunifu huyo wa programu ya SKY AI
Emmy anasema App hiyo ya Akili Mnemba imepokelewa vyema na wadau wa usafiri wa anga. Anasema wamefurahishwa na mapokeo hayo makubwa na ya kuridhisha.
SKY AI imeshaanza kufanya kazi na makampuni
Kwa sasa App ya SKY AI inatumika katika ngazi mbili tofauti, ikiwemo katika makampuni na katika ngazi ya wataalamu. SKY AI tayari wameshasaini mkataba wa mwaka mzima na mashirika mawili ya ndege ambayo yanatumia mfumo wa programu hiyo kikamilifu.
”Zaidi ya hayo tunafanya majaribio na shirika mojawapo ambalo ndilo yenye idadi kubwa ya ndege. Hii inaonesha imani kubwa ambayo wadau wanayo kwetu,” alifafanua Emma.
Aidha, SKY AI amekuwa msaidizi mkubwa kwa wataalamu binafsi wa mashirika makubwa na hata wafanyakazi wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga, TCAA.
Isaac Ruto, mdau wa masuala ya usalama wa anga, anasema SKY AI imefanikiwa kuwasaidia hususan katika miongozi wanaoitumia. Hata hivyo kulingana na Isaac, programu hiyo ya Akili Mnemba inaweza kuboreshwa zaidi kubashiri hatari zinazoweza kujitokeza kutokana na mwenendo wa shughuli za kampuni ya ndege.
”Ningependa kuona SKY AI ikiongeza uwezo wa kuchataka taarifa za kiusalama zinazotarajiwa kutokea, yaani mfumo uweze kuchakata ripoti zote za nyuma na kubaini mienendo kabla ya kutokea tukio,” alisisitiza Isaac.
Waswahili wanasema hatua moja huanzisha nyingine, mipango ya SKY AI ni kuwafikia watu wengi zaidi. Kwa mujibu wa Emma, mipango iliyopo kwa sasa ni kuhakikisha programu ya SKY AI inafika mbali zaidi ndani na nje ya nchi, ili kuendelea kurahisisha shughuli za usafiri wa anga na kuendelea kutoa uhakika wa usalama wa usafiri huo unaokuwa kwa kasi katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Lengo la kuwafikia watu wengi zaidi
”Dira yetu ni kuhakikisha SKY AI inagusa kila nyanja ya anga kuanzia udhibiti wa mazingira hadi uwezeshaji wa kifedha. Tuna mipango mikakati minne, kuimarisha mifumo ya udhibiti na elimu, na tunatengeneza mfumo maalumu kwa ajili ya TCAA ili kuongeza ufanisi wao katika usimamizi,” alibainisha Emma.
Emma anasema vile vile wanashirikiana na vyuo vya anga kuanzisha shule ya anga inayoendeshwa na AI, ili kuzalisha wataalam bora kwa haraka zaidi. Aidha, wanaangalia upanuzi wa kimataifa kwamba anga halina mipaka. Tayari wapo katika mazungumzo na mashirika ya nchini Kenya, kwani suluhisho la SKY AI linaweza kufanya kazi popote duniani.
App ya SKY AI ni mojawapo ya programu nyingi za Akili Mnemba zinazotengenezwa na vijana wa Kitanzania ikiwa ni sehemu ya kutumia teknolojia kutatua changamoto zinazoizunguka jamii.
Makala hii imeandaliwa na Anuary Mkama
