Rais wa Marekani Donald Trump alitangaza Jumatatu kwamba nchi zinazofanya biashara na Iran zitakabiliwa na ushuru wa asilimia 25 kutoka Marekani. Trump alitangaza ushuru huo katika chapisho la mitandao ya kijamii, akisema “utaanza kutumika mara moja.”
“Kuanzia mara moja, nchi yoyote inayofanya biashara na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran italipa ushuru wa 25% kwa biashara yoyote inayofanywa na Marekani,” Trump aliandika. “Agizo hili ni la mwisho.”
Ilikuwa hatua ya kwanza ya moja kwa moja dhidi ya Iran kwa ajili ya msako na ukandamizaji wa maandamano kutoka kwa Trump, ambaye anaamini kutoza ushuru kunaweza kuwa chombo muhimu katika kuwashawishi marafiki na maadui duniani kote kukubali mapenzi yake.
Brazil, China, Uturuki, Umoja wa Falme za Kiarabu na Urusi ni miongoni mwa nchi zinazofanya biashara na Iran. Ikulu ya White House ilikataa kutoa maoni zaidi kuhusu tangazo la ushuru la rais.
Trump asema Iran yataka mazungumzo
Rais wa Marekani Donald Trump amesema Iran inataka kujadiliana na Marekani baada ya tishio lake la kuishambulia Jamhuri hiyo ya Kiislamu kutokana na ukndamazijai wake dhidi ya waandamanaji katika maandamano ya kitaifa ambayo wanaharakati walisema Jumatatu yamewaacha watu wasiopungua 599 wakiwa wamekufa.
Ikulu ya White House inasema rais Trump anafikiria kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya Iran ili kusimamisha msako wake dhidi ya maandamano, lakini njia ya diplomasia bado iko wazi.
Iran haikuwa na majibu ya moja kwa moja kwa maoni ya Trump, ambayo yalikuja baada ya waziri wa mambo ya nje wa Oman, ambaye kwa muda mrefu alikuwa mzungumzaji kati ya Washington na Tehran, kusafiri hadi Iran wikendi hii. Pia bado haijulikani ni nini hasa Iran inaweza kuahidi, hasa kwani Trump ameweka madai makali kuhusu mpango wake wa nyuklia na silaha zake za makombora ya masafa marefu, ambayo Iran inasisitiza kuwa ni muhimu kwa ulinzi wake wa kitaifa.
Waziri wa mambo ya nje wa Iran Abbas Araghchi, akizungumza na wanadiplomasia wa kigeni mjini Tehran, alisisitiza kuwa hali imedhibitiwa kabisa katika matamshi yaliyoilaumu Israeli na Marekani kwa vurugu hizo, bila kutoa ushahidi.
Hata hivyo, Araghchi alisema Iran ilikuwa “wazi kwa diplomasia.” Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Iran, Esmail Baghaei, alisema kwamba njia ya kuelekea Marekani bado iko wazi, lakini mazungumzo yanahitajika “kuzingatia kukubalika kwa maslahi na wasiwasi wa pande zote mbili, si mazungumzo ya upande mmoja na yanayotegemea imla.”
Trump akubali pendekezo la mazungumzo
Trump na timu yake ya usalama wa taifa wamekuwa wakipima majibu mbalimbali yanayowezekana dhidi ya Iran, ikiwa ni pamoja na mashambulizi ya mtandaoni na mashambulizi ya moja kwa moja kutoka Marekani au Israel, kulingana na watu wawili wanaofahamu mijadala ya ndani ya Ikulu ya White House ambao hawakuruhusiwa kutoa maoni hadharani na waliozungumza kwa sharti la kutotajwa majina.
“Jeshi linaangalia hilo, na tunaangalia mapendekezo ya hatua kali sana,” Trump aliwaambia waandishi wa habari katika ndege ya Air Force One Jumapili usiku. Alipoulizwa kuhusu vitisho vya kulipiza kisasi vya Iran, alisema, “Ikiwa watafanya hivyo, tutawapiga kwa viwango ambavyo hawajawahi kupigwa hapo awali.”