Umoja wa Mataifa umewatolea wito viongozi wa Iran kukomesha matumizi ya nguvu dhidi ya watu wanaondamana kwa amani. Jeremy Laurence, Msemaji wa Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa (OHCHR) ametoa wito kwa serikali ya Iran kwa kusema mauaji ya watu wanaoandamana kwa amani lazima yakome, na kwamba jambo la kuwaita waandamanaji ‘magaidi’ ili kuhalalisha vurugu dhidi yao halikubaliki.
” Tunazitaka mamlaka za Iran kusitisha mara moja vurugu zote na ukandamizaji dhidi ya waandamanaji na kurejesha mtandao wa intaneti na huduma za mawasiliano,” alisema Laurence.
Wakati huohuo, Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen amesema Jumanne kuwa wanatathmini vikwazo vipya kwa Iran hasa wakati huu idadi ya vifo kufuatia maandamano ya kuipinga serikali ikiongozeka. Kauli ya von der Leyen imethibitishwa na Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Kaja Kallas.
Von der Leyen amesema Umoja wa Ulaya unawaunga mkono raia wa Iran wanaotetea haki zao kwa ujasiri na kwamba idadi inayoongezeka ya wahanga inatisha huku akilaani matumizi ya nguvu kupita kiasi na kuendelea kuwekwa kwa vizuizi vinavyokandamiza uhuru wa raia, na kusisitiza kuwa “vikwazo zaidi kwa wale waliohusika na ukandamizaji vitapendekezwa haraka.”
Kwa siku kadhaa sasa, mamlaka za Iran zilifunga mawasiliano na kuzima kabisa mtandao wa intaneti. Hata hivyo leo hii wamelegeza baadhi ya vizuizi kwa raia wake na kuwaruhusu kupiga simu za kimataifa kupitia simu zao za mkononi.
Iran yajibu vikali kauli ya Kansela wa Ujerumani
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi alijibu vikali kauli ya Kansela wa Ujerumani, Friedrich Merz, aliyesema hivi leo kuwa utawala wa Iran unaishi siku zake za mwisho.
Araghchi amesema Ujerumani inapaswa kukomesha uingiliaji wake katika eneo hilo na kwamba ipo katika nafasi mbaya zaidi kuzungumzia masuala ya ‘haki za binadamu,’ hasa kutokana na undumilakuwili iliouonyesha na uliofuta uaminifu wake kwa kuiunga mkono Israel wakati wa vita vya Gaza.
Kulingana na Merz , mawaziri wa mambo ya nje wa Ujerumani, Marekani, Uingereza na Ufaransa wapo “katika mawasiliano ya karibu ili kuhakikisha kunapatikana serikali ya mpito ya amani nchini Iran kuelekea utawala halali wa kidemokrasia.”
Idadi ya vifo yaongezeka huko Iran
Shirika la kutetea haki za binaadamu la Iran (IHRNGO) lenye makao yake makuu mjini Oslo limesema kuwa watu wasiopungua 648 wameuawa tangu kuanza kwa maandamano hayo mwezi Desemba 28 mwaka jana.
Shirika hilo limeendelea kueleza kuwa kuna taarifa zinazokadiria kuwa idadi ya vifo huenda ikafikia karibu watu 6,000, huku wengine zaidi ya 10,000 wakiaminika kukamatwa.
Iran imekuwa ikikabiliwa na wimbi kubwa la maandamano yaliyoanza kama malalamiko ya wafanyabiashara kutokana na kushuka thamani sarafu ya Iran ya “rial” pamoja na mdororo wa kiuchumi.
Baadaye madai hayo yaligeuka kuwa maandamano ya kitaifa ya kuupinga utawala. Serikali mjini Tehran imekuwa ikiyatuhumu mataifa ya kigeni yakiongozwa na Marekani na Israel kwa kuchochea maandamano hayo.
