
Jeshi la Israel limesema limerejesha mwili wa mateka wa mwisho aliyebaki Gaza. Lilikuwa likimtafuta Sajenti Ran Gvili tangu usiishaji wa mapigano na Hamas kuanza mwezi Oktoba.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Hamas ilikusudiwa kuwarejesha mateka wote, wakiwa hai na waliokufa, ndani ya saa 72 baada ya usitishaji mapigano kuanza. Mateka 20 wa Israel walio hai na miili ya mateka 27 wa Israel na wageni waliofariki ilikabidhiwa lakini kwa wiki chache zilizopita Hamas ilisema bado haijaweza kumpata Gvili.
Siku ya Jumapili, Israel ilisema itafungua tena mpaka muhimu wa Gaza na Misri mara tu operesheni ya kumtafuta na kumrudisha Gvili itakapokamilika.
Kupatikana kwa mwili wa Gvili kunafungua njia kwa Israel na Hamas kusonga mbele hadi awamu ya pili ya mpango wa amani wa Donald Trump.
Awamu ya pili inakusudiwa kuhusisha ujenzi mpya na kuondoa kabisa wanajeshi wa Israel huko Gaza, ikiwa ni pamoja na kupokonya silaha wanamgambo wa Hamas na makundi mengine ya Wapalestina.
Israel ilikuwa imepinga hatua zote hadi ipate mwili wa Gvili.
Katika taarifa, Jeshi la Ulinzi la Israel limesema: “Kulingana na taarifa na ujasusi tulio nao, Sajenti Ran Gvili … mpiganaji wa kikosi cha Yamam, mwenye umri wa miaka 24 wakati wa kifo chake, aliauawa vitani asubuhi ya Oktoba 7, 2023, na mwili wake ukatekwa nyara hadi Ukanda wa Gaza.
“Jeshi la Israel linashiriki huzuni ya familia. Litaendelea kuzisaidia familia na mateka walioachiliwa na kuchukua hatua ya kuimarisha usalama wa raia wa Israel”, jeshi limesema.
“Kwa hili, mateka wote kutoka eneo la Ukanda wa Gaza wamerudishwa”, jeshi limeongeza katika taarifa.