
Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika jana Ijumaa alitoa wito kwa pande zinazozozana kujiepusha na mivutano haraka iwezekanavyo baada ya vyombo vya habari kuripoti kwamba safari za ndege zimesimamishwa katika eneo la Tigray kaskazini mwa Ethiopia safari za ndege kutokana na mapigano ya silaha yaliyoibuka katika eneo hilo.
Mahmoud Ali Youssouf amesema haya baada ya wanaharakati na vyama vya kisiasa katika eneo la Tigray, kaskazini mwa Ethiopia, kupaza sauti wakitaka kujiepusha na vita katika eneo la Tigray.
Salsay Woyane, chama cha upinzani katika eneo la Tigray, kimeandika barua ya wazi kikiwatahadharisha wapatanishi kuhusu uwezekano wa kusambaratika vibaya amani inayolegalega ya Tigray.
Chama hicho kimetoa wito wa kufanyika juhudi za haraka za kidiplomasia kati ya Serikali ya Shirikisho ya Ethiopia na Harakati ya Ukombozi ya Watu wa Tigray (TPLF) ili kuliepusha eneo hilo kutumbukia katika maafa mengine.
Ripoti za vyombo vya habari zinasema kuwa hali ya usalama ilibadilika siku ya Alkhamisi wakati Shirika la Ndege la Ethiopia liliposimamisha ghafla safari zote za ndege zilizokuwa zimepangwa kuelekea Mekelle, makao makuu ya mkoa wa Tigray pamoja na huko Axum, Shire na Humera.
Wakati huo huo mapigano mapya yameripotiwa katika eneo la Tselemti magharibi mwa Tigray; eneo lililosalia na ukosefu wa usalama tangu kumalizika rasmi vita vya ndani.
Mvutano wa sasa huko Tigray kaskazini mwa Ethiopia ni mtihani mkubwa kwa Mkataba wa Kusimamisha Kikamilifu Vita (COHA), uliotiwa saini mjini Pretoria, Afrika Kusini mwezi Novemba 2022.
Licha ya makubaliano haya kuhitimisha mzozo wa miaka miwili kati ya serikali ya shirikisho ya Ethiopia na Harakati ya Tigray People’s Liberation Front, mizozo kuhusu maeneo yanayogombaniwa na mamlaka zote mbili za Tigray na Amhara inaendelea kuzorotesha mchakato huo wa amani.