Kiashiria muhimu cha shughuli za uzalishaji za China kimepungua kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miezi miwili. Lawama kubwa inawekwa kwenye mahitaji ya ndani yasiyoongezeka kutokana na kushuka kwa muda mrefu kwa soko la mali isiyohamishika nchini humo.
Kushuka kwa kipimo hicho kulikuja baada ya kuashiria ongezeko la kwanza katika miezi tisa mwezi Desemba, wakati Marekani ikipunguza kwa kiasi ushuru wa forodha wa ziada kwa China mwezi Novemba.
Kipimo cha Mameneja wa Ununuzi au PMI kwa mwezi Januari kilikuja kwa alama 49.3. Hiyo ni chini kwa alama 0.8 kutoka mwezi uliopita.
Ofisi ya Kitaifa ya Takwimu iliwahoji wazalishaji 3,200 katika kukusanya faharisi. Takwimu zilizo juu ya 50 zinawakilisha ukuaji huku zile zilizo chini zikionyesha kupungua.
Kiwango cha makampuni makubwa kwa Januari kilikuwa 50.3, lakini makampuni ya ukubwa wa kati kilikuwa 48.7, na makampuni madogo kilikuwa 47.4.
Kipimo cha makampuni yasiyokuwa ya uzalishaji, ikiwa ni pamoja na watoa huduma, kilikuwa 49.4.
Serikali ya China inaweka kipaumbele cha juu katika upanuzi wa mahitaji ya ndani. Wachumi wanasubiri kuona kama serikali itaweza kuchukua hatua madhubuti kwa makampuni ili kuboresha hisia zao za kibiashara.