
Serikali ya Marekani imeidhinisha mauzo ya silaha zenye thamani ya dola bilioni 6.67 kwa utawala wa kizayuni wa Israel wakati huu ambapo kuna usitishaji mapigano unaolegalega katika vita vya mauaji ya kimbari vilivyoanzishwa na utawala huo haramu dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Ghaza.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imetangaza kuwa Israel imeidhinishiwa kununua silaha zilizotengenezwa na Marekani, ikiwa ni pamoja na helikopta 30 za mashambulizi za Apache kwa dola bilioni 3.8 na vifaru vya mashambulizi vyenye thamani ya dola bilioni 1.98.
Vikosi vya jeshi la utawala wa kizayuni vimetumia sana helikopta za Apache kuwafyatulia risasi na kuwaua Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi na Ukanda wa Ghaza, ambapo hadi sasa 71,662 miongoni mwao wameuawa shahidi katika vita vya kinyama vya mauaji ya kimbari vilivyoanzishwa na utawala huo tangu Oktoba 2023.
“Marekani imejitolea kwa ajili ya usalama wa Israel, na ni muhimu sana kwa maslahi ya taifa ya Marekani kuisaidia Israel kukuza na kudumisha uwezo imara na wenye utayari wa kujilinda,” imeeleza taarifa wizara ya mambo ya nje ya Marekani.
Taarifa hiyo imeongezea kwa kusema: “uuzaji huu uliopendekezwa unaendana na malengo hayo”.
Marekani huwa kila mwaka inaipelekea pia Israel zana za kijeshi zenye thamani ya mabilioni ya dola, zana na silaha ambazo kwa kiasi kikubwa hutolewa zaidi kama msaada badala ya kuwa za mauzo.
Mashirika ya kutetea haki za binadamu na wataalamu wa Umoja wa Mataifa wamekuwa kila mara wakiitaka Marekani isimamishe kuipelekea silaha Israel, ambazo wanasema zimezidisha uwezo wa kijeshi wa utawala huo wa kizayuni wa kuendesha vita vya mauaji ya kimbari huko Ghaza…/