
Askari wasiopungua 10 na magaidi 109 wameuawa katika mapigano wakati vikosi vya usalama vya Pakistan vilipozima mashambulizi makubwa “yaliyoratibiwa” katika jimbo la kusini-magharibi mwa Balochistan. Hayo yalielezwa jana Jumamosi na afisa mmoja wa usalama wa Pakistan.
Afisa huyo mwandamizi wa usalama ambaye amezungumza na vyombo vya habari kwa sharti la kutotajwa jina amesema, magaidi walifanya mashambulizi yaliyoratibiwa katika maeneo 12 tofauti kote mkoani Balochistan, ikiwa ni pamoja na makao makuu ya mkoa Quetta.
“Wanamgambo walilenga maeneo mengi, ikiwa ni pamoja na vituo vya vikosi vya usalama huko Quetta, Noshki, Dalbandin, Pasni, na Gwadar,” ameeleza afisa huyo.
Ameongeza kuwa vikosi vya jeshi la Pakistan, Frontier Corps, na Polisi wa Balochistan walichukua hatua haraka kuzuia kile alichokielezea kama “mipango mibaya” ya magaidi.
Kwa mujibu wa maafisa, magaidi 58 waliuawa wakati wa operesheni za Jumamosi, na wengine 51 waliuawa katika operesheni tofauti za kiusalama kote mkoani siku ya Ijumaa, na kufikisha jumla ya vifo 109 katika saa 48 zilizopita.
Wakati wa mapigano hayo, maafisa 10 wa usalama pia walipoteza maisha, na wengine kadhaa walijeruhiwa.
Siku ya Ijumaa, jeshi la Pakistan lilitangaza kuwa, magaidi wasiopungua 41 waliuawa katika operesheni mbili tofauti za kiusalama katika wilaya za Harnai na Panjgur za Balochistan.
Pakistan imeshuhudia ongezeko jipya la machafuko katika miaka ya hivi karibuni, hususan katika maeneo yake ya magharibi na kusini-magharibi…/