Mahakama ya Hong Kong imefanya kikao chake cha kwanza kuhusu wizi wa barabarani wa zaidi ya yeni milioni 50, au takriban dola za Marekani 330,000, unaowahusisha raia wa Japani.
Wajapani watatu na Mchina mmoja wameshtakiwa kwa madai ya kula njama ya kumnyang’anya mwanaume wa Kijapani mwenye umri wa miaka 51, takriban yen milioni 51 Januari 30 katika mtaa wa burudani huko Hong Kong.
Washtakiwa hao wanne walifika mahakamani Februari 2, na kusikiliza usomaji wa hati ya mashtaka.
Polisi wa Hong Kong wanasema mmoja wa washtakiwa, Suzuki Yusuke, mwenye umri wa miaka 27, alisafirisha takriban yeni milioni 190, au zaidi ya dola milioni 1.2 za Marekani, pesa taslimu hadi Hong Kong akiwa na mwathiriwa.
Wakati wa kikao hicho, waendesha mashtaka walisema picha za kamera za usalama wa teksi zilionyesha mwathiriwa akiwazuia wanyang’anyi, huku Suzuki akionyesha kutochukua hatua kuzilinda pesa hizo. Kesi kamili inatarajiwa kusikilizwa Aprili.
Mwanamume huyo wa Kijapani mwenye umri wa miaka 51, anaaminika pia alishambuliwa katika jaribio la wizi lililoshindwa katika maegesho ya magari ya Uwanja wa Ndege wa Haneda jijini Tokyo, kabla ya kuondoka kwenda Hong Kong mapema Januari 30. Pesa hizo hazikuibwa.
Polisi wanaamini gari lililopatikana kwenye ukingo wa mto katika mkoa wa Kanagawa lilikuwa gari lililotumiwa kutoroka na watu wanne waliohusika katika shambulio hilo lililofanyika katika uwanja wa ndege. Polisi wanaamini kwamba wahusika bado wako nchini Japani.