Utawala wa Rais Trump umekuwa ukiongeza shinikizo kwa Iran kuingia katika mazungumzo kuhusu mpango wake wa nyuklia.
Chombo cha habari cha Marekani cha Axios kinaripoti kwamba mazungumzo juu ya nyuklia kati ya Marekani na Iran yanatarajiwa kufanyika nchini Uturuki baadaye wiki hii.

Kilivinukuu vyanzo vingi katika habari iliyochapishwa Februari 2. Vyanzo hivyo vilisema kwamba mjumbe maalum wa Rais Donald Trump, Steve Witkoff anatarajiwa kukutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi jijini Istanbul Februari 6, na wanapanga kujadili uwezekano wa makubaliano ya nyuklia.

Mkwewe Trump Jared Kushner, atahudhuria, pamoja na mawaziri wa mambo ya nje wa nchi kadhaa za Kiarabu na Kiislamu.

Ripoti hiyo ilimnukuu afisa mmoja wa Marekani akisema kwamba mkutano huo utazingatia kuandaa “mpango mzima unaozuia vita.” Axios ilisema mkutano huo ni matokeo ya shinikizo la kidiplomasia la Uturuki, Misri na Qatar katika siku kadhaa zilizopita.

Vyombo vya habari vya serikali ya Iran pia viliripoti kwamba Rais wa nchi hiyo Masoud Pezeshkian ameagiza mazungumzo mapya na Marekani.

Lakini mapengo makubwa yanasalia. Ripoti hiyo ilisema utawala wa Trump unadai kwamba makubaliano yoyote yajumuishe mipango ya nyuklia na makombora ya Iran, pamoja na washirika wa kikanda, lakini Iran inataka kuangazia suala la nyuklia lililo mezani pekee.

Inasemekana huu utakuwa mkutano wa kwanza kati ya pande hizo mbili tangu mazungumzo yalipovunjika na mapigano kutokea mwezi Juni mwaka jana.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *