Kundi la wanamgambo limefanya mashambulizi yaliyoratibiwa katika jimbo la kusini magharibi mwa Pakistan la Balochistan, na kusababisha vifo vya askari 17 wa vikosi vya usalama na raia 31. Vikosi vya usalama vinasema baadaye viliwaua wapiganaji wengi.

Jeshi la Ukombozi la Balochistan, BLA lilidai kuhusika. Kundi hilo la waasi linatafuta uhuru kutoka Pakistan.

Mashambulizi dhidi ya vituo vya kijeshi na polisi yalifanyika Januari 31 katika miji na vijiji tisa.

Mlinzi wa benki alisema kwamba saa 8:30 usiku, wapiganaji wa BLA walivunja madirisha na milango, waliingia na kumshambulia. Alisema wafanyakazi waliambiwa wavue sare zao na walilazimishwa kutoka nje ya benki baada ya kufanya hivyo.

BLA imeongeza shughuli zake katika miaka ya hivi karibuni. Mwezi Machi mwaka jana, wapiganaji wake walishambulia treni iliyokuwa imebeba abiria wapatao 400 na kuwaua watu 25.

Kabla na baada ya mashambulizi ya hivi karibuni, jeshi na polisi wa Pakistan walianzisha operesheni za kupambana na ugaidi, na kuwaua zaidi ya wanamgambo 170 katika siku tatu za mapigano.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *