Morogoro. Mkurugenzi wa Bendi ya Tanzania One Theatre (TOT), Khadija Kopa amesema mwimbaji na mtunzi wa taarabu, Ally Star anazikwa leo Kilosa mkoani Morogoro, lakini akigusia pia namna kundi hilo lilivyopoteza muasisi mwingine.

TOT ilianzishwa miaka ya mwanzoni mwa 1990 ambapo mmoja wa waanzilishi wake na mkurugenzi wa kwanza wa kundi hilo alikuwa Kepteni John Komba, ambaye pia alishatangulia mbele za haki.

Akizungumza na Mwananchi, Kopa amesema alimfahamu Ally Star tangu alipojiunga na kundi hilo mwaka 1992, na ni mmoja wa waanzikishi hivyo walifanya kazi kwa karibu kwa miaka mingi katika kujenga bendi.

“Ally Star alikuwa mtu wangu wa karibu sana. Tulianza kazi pamoja TOT tangu 1992, alikuwa msanii mwenye nidhamu, kipaji na mapenzi makubwa kwa sanaa,” amesema Kopa.

Amesema mwanamuziki huyo alianza kuumwa mbavu na kifua tangu Julai, mwaka jana tatizo la kiafya ambalo lilihusishwa pia na ajali waliyowahi kupata awali.

Kopa amesema hali hiyo ilianza taratibu kabla ya afya yake kuzorota zaidi kadri muda ulivyokuwa unaenda.

Ameongeza kuwa baadaye Ally Star alipata kiharusi  kidogo na kuwalazimu kumpeleka Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa ajili ya matibabu. 

Kwa mujibu wa Kopa, baada ya siku chache akiwa hospitali hali yake ilianza kuimarika kidogo, jambo lililoipa familia matumaini pamoja na wasanii wenzake.

“Alikuwa anaendelea vizuri kidogo tukapata matumaini, lakini ghafla akapatwa na mauti. Tumelipokea hili kama mapenzi ya Mwenyezi Mungu,” amesema. 

Kopa amesema kifo cha Ally Star kimeacha pengo  ndani ya TOT, akisisitiza kuwa mchango wake kama mwanzilishi, mwimbaji na mtunzi utaendelea kukumbukwa kupitia nyimbo, maadili na historia ya bendi hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *