Morogoro. Msanii wa muziki wa taarabu na Bendi ya Tanzania One Theatre (TOT), Abdul Misambano amezungumzia kifo cha mwimbaji na mtunzi wa taarabu, Ally Star.

Akizungumza na Mwananchi, Misambano amesema Ally Star alikuwa msanii aliyependa furaha na aliyeleta mwanga ndani ya bendi, hali iliyomfanya aheshimiwe na kupendwa na wengi.

Amesema pamoja na utani na ucheshi wake, Ally Star alikuwa mtu wa nidhamu na aliyeheshimu kazi na jukwaa la sanaa.

Msanii huyo amesema dalili za kuumwa kwa Ally Star zilianza kujitokeza kabla za kampeni uchaguzi mkuu mwaka jana, ambapo alianza kulalamika kuhusu hali yake ya afya. Hata hivyo, baada ya kampeni kumalizika, afya yake ilizorota zaidi kiasi cha kuhitaji matibabu kutoka kwa wataalamu wa afya.

“Ally Star ameanza kuumwa miezi minne iliyopita kabla hata ya kampeni za uchaguzi, hivyo katika kampeni hatukuwa naye. Tumemaliza kampeni mkurugenzi wa TOT Khadija Kopa alinipigia simu twende tukamuone,” amesema Misambano na kuongeza:

“Tulipofika nyumbani kwake hatukumkuta na hali nzuri ndipo Khadija Kopa akasema tumpeleke katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa ajili ya matibabu. Muhimbili amekaa wiki tatu na nusu ndio amefariki jana.”

Akizungumzia tatizo lililokuwa likimsumbua Ally Star, mwanamuziki huyo amesema alipatwa na kiharusi (stroke)’ na alikutwa na ukungu kwenye kifua.

Misambano amesema alimfahamu Ally Star tangu 1993 alipojiunga na Bendi ya TOT na tangu wakati huo alionyesha mapenzi makubwa katika muziki wa taarabu akijituma kwa dhati kuitumikia sanaa hiyo.

Amesema kifo cha msanii huyo ni pigo kubwa kwa TOT pamoja na tasnia ya muziki wa taarabu akisisitiza kuwa kazi alizoziacha zitaishi kupitia nyimbo alizoimba na kutunga pamoja na maadili na mshikamano aliowaachia wasanii wenzake.

Ally Star alifariki dunia Januari 3, 2026 katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na leo mwili wake unasafirishwa kwenda kuzikwa nyumbani kwao Kichangani wilayani Kilosa, Mkoa wa Morogoro.

Hata hivyo kwa upande wake mwanamuziki Thabit Abdul amesema kwa Ally Star alikuwa anajifunza vitu vingi ikiwemo utunzi na  upigaji kinanda kwani alikuwa makini kila alipokuwa akitoa nyimbo anamsikiliza.

“Ally Star alikuwa mtu wa kucheka na kila mtu. Ukikaa naye dakika mbili lazima ucheke, lakini pia alikuwa mshauri mkubwa wa wasanii wengi. Mimi nimejifunza sana utunzi kupitia nyimbo zake, na upigaji wa kinanda, kutoka kwake,” amesema Thabit.

Amesema pengo lililobaki baada ya kifo cha Ally Star ni gumu kuliziba, lakini bado kuna wasanii wanaoweza kuiga yaliyomo ndani ya kipaji cha mwanamuziki huyo.

 “Pengo la Ally Star kuliziba ni ngumu, lakini bado tunaweza kupata wasanii wenye kipaji cha aina hiyo, ingawa si rahisi kama yeye,” amesema.

Ameongeza kuwa ndani ya TOT Ally Star atabaki kuwa nguzo muhimu ya mafanikio yao, huku akiwaachia ucheshi, urafiki na ushauri vitu alivyokuwa navyo.

Mwanamuziki huyo alifariki dunia jana, Januari 3,  2026 katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na leo anasafirishwa kwenda kuzikwa nyumbani kwao Kichangani, Kilosa mkoani Morogoro.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *