Chanzo cha picha, Reuters
Saif
al-Islam Gaddafi, mwana wa kiongozi wa zamani wa Libya Kanali Muammar Gaddafi,
ameripotiwa kupigwa risasi na kuuawa.
Kifo cha
mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 53, ambaye hapo awali alionekana kuwa
mrithi wa baba yake, kilithibitishwa na mkuu wa timu yake ya kisiasa siku ya
Jumanne, kulingana na Shirika la habari la Libya.
Wakili wake
aliambia shirika la habari la AFP kwamba kikosi cha “makomandoo
wanne” kilifanya mauaji nyumbani kwake katika jiji la Zintan, ingawa
haikuwa wazi ni nani aliyehusika na shambulio hilo.
Hata hivyo,
dada yake alitoa taarifa zinazokinzana na hizo akiambia televisheni ya Libya
kwamba alifariki karibu na mpaka wa nchi hiyo na Algeria.
Saif
al-Islam Gaddafi kwa muda mrefu alionekana kama mtu mwenye ushawishi mkubwa na
anayeogopwa zaidi nchini baada ya baba yake, ambaye alitawala Libya kuanzia
1969 hadi alipoondolewa madarakani na kuuawa wakati wa uasi mwaka 2011.
Alizaliwa
mwaka wa 1972 na kuchukua jukumu muhimu katika uhusiano wa Libya na nchi za
Magharibi kuanzia mwaka wa 2000 hadi kuanguka kwa utawala wa Gaddafi.
Baada ya
kuondolewa kwa baba yake, Saif al-Islam Gaddafi – ambaye alishutumiwa kwa
kuchukua jukumu muhimu katika ukandamizaji wa kikatili wa maandamano ya kupinga
serikali – alifungwa jela na wanamgambo wapinzani katika jiji la Zintan kwa
karibu miaka sita.
Mahakama ya
Kimataifa ya Jinai ilitaka kumshtaki kwa uhalifu dhidi ya ubinadamu kwa madai
ya jukumu lake katika kukandamiza maandamano ya upinzani mwaka wa 2011.
Mnamo mwaka
wa 2015, alipewa hukumu ya kifo bila kuwepo mahakamani na mahakama ya Libya kwa
jukumu lake katika msako huo.
Gaddafi
alikuwa akikana kila mara kwamba alitaka kurithi madaraka kutoka kwa baba yake,
akisema hatamu za madaraka hazikuwa “shamba la kurithi”.
Hata hivyo,
mwaka wa 2021 alitangaza kwamba angegombea urais katika chaguzi ambazo baadaye
ziliahirishwa kwa muda usiojulikana.
Soma zaidi: