
Mtu aliyefariki miaka mitano iliyopita ameteuliwa katika kamati iliyopewa jukumu la kuandaa uchaguzi nchini Sudan Kusini, na kusababisha kejeli nyingi kwenye mitandao ya kijamii na kuilazimisha serikali kuomba radhi. Rais Salva Kiir alimfukuza kazi katibu wake wa habari na mkurugenzi mkuu kwenye Wizara ya Mambo ya Nje. Familia ya marehemu inadai “fidia ya kimaadili na kitamaduni.”
Imechapishwa:
Dakika 2 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Nchini Sudan Kusini, Rais Salva Kiir na timu yake wanakabiliwa na kejeli baada ya mwanamume aliyefariki miaka mitano iliyopita kuteuliwa kusaidia kupanga chaguzi zijazo. Mtu huyo alikuwa mwanachama wa chama cha upinzani cha United Democratic Party (UDP) na alipangwa kujiunga na kamati inayojiandaa kwa uchaguzi uliopangwa kufanyika mwezi Desemba 2026.
Hati rasmi ilimtaja Steward Sorobo miongoni mwa wanachama wa kamati iliyopewa jukumu la kuandaa chaguzi hizo. Vyombo vya habari vya eneo hilo viliharakia kuripoti kifo chake, ambacho kilisababisha kejeli mtandaoni, pamoja na maoni kwenye mitandao ya kijamii kama vile “Tumweke Steward Sorobo kama mratibu kati ya wafu na walio hai.”
Familia inadai “fidia kwa kusumbua roho” ya marehemu
Katika taarifa, mamlaka zimejitetea dhidi ya shutuma za kosa la kiutawala na kuahidi kurekebisha tukio hilo. Lakini “mabadiliko rahisi ya jina” hayatoshi, inasema familia, ambayo inadai fidia ya kimaadili na kitamaduni. Fidia ya kimaadili kwa sababu tukio hilo limewasababishia “kuingliwa tena huzuni na kuanza kuomboleza upya,” waliandika katika barua kwa ofisi ya rais, iliyonukuliwa na kituo cha redio cha Tamazuj. Na fidia ya kitamaduni kwa sababu, katika utamaduni wao, waliandika, “haikubaliki kuamsha au ‘kushtua’ roho na nafsi ya marehemu bila idhini ya familia.” Kwa hivyo wanadai “fidia inayofaa kwa kusumbua roho ya mwanasiasa aliyefariki,” kulingana na mila zao.
Sudan Kusini, taifa changa zaidi duniani, ambalo lilipata uhuru wake kutoka Sudan mwaka wa 2011, halijawahi kufanya uchaguzi hata mmoja. Nchi hiyo ilitumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe kati ya mwaka 2013 na 2018. Mkataba wa amani uliosainiwa mwaka wa 2018 ulizileta pande zinazopigana pamoja, lakini zimeshindwa mara kwa mara kupanga uchaguzi ulioainishwa katika makubaliano.
Uchaguzi uliopangwa kufanyika mwaka 2024 ulisogezwa mbele hadi mwezi Desemba 2026, lakini wachambuzi wengi wana shaka kwamba chaguzi hizo huenda zisifanyiki kwa tarehe hiyo, kutokana na wimbi jipya la vurugu nchini humo.