
Baada ya Shirik la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani, Save the Children pia imesitisha shughuli zake mashariki mwa Sudan Kusini, kuanzia siku ya Alhamisi. Shirika hilo lisilo la kiserikali limetangaza kusitisha kwa muda shughuli zake na kuwahamisha wafanyakazi wake 30 katika Jimbo la Jonglei baada ya mfululizo wa mashambulizi dhidi ya vituo vyake, na kuwanyima mamia ya watoto na familia huduma ya afya.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Shirika hilo lisilo la kiserikali linasema kwa hivyo linalazimika kusitisha shughuli zake. Save the Children inaripoti ofisi kuchomwa moto, kituo cha afya kuharibiwa, na magari manne kuibiwa na makundi yenye silaha.
Katika eneo hili, mamia ya wakazi wanakimbia eneo hilo na kuishi katika mazingira ya kutisha, kulingana na shirika hilo, ambalo linahesabu zaidi ya watu 235,000 waliokimbia makazi yao katika wiki nne ili kuepuka vurugu katika Jimbo la Jonglei. Eneo hilo, ambalo ni kubwa zaidi nchini, ni eneo linalokumbwa na mapigano ya vurugu kati ya vikosi vya serikali na makundi ya upinzani yenye silaha na wanamgambo wa eneo hilo, huku kukiwa na ukosefu wa usalama ulioenea. Pia ni eneo lililoathiriwa zaidi na ukosefu wa usalama wa chakula.
Tangazo hili linakuja muda mfupi baada ya lile la Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani, ambao lilisitisha shughuli zake mnamo Februari 1 katika Jimbo la Upper Nile, kaskazini zaidi, kufuatia shambulio na uporaji kwenye msafara wa majini. Katika Jimbo la Jonglei, shirika la Umoja wa Mataifa linasema haliwezi kuwasilisha tani 12,000 za chakula kutokana na vikwazo vya serikali vya kuingia nchii humo.
Katika eneo hilo, Shirika llisilo la kiserikali la Madaktari Wasio na Mipaka pia lililazimika kuhamisha timu zake na kusitisha huduma ya matibabu katika maeneo kadhaa baada ya hospitali kushambuliwa na kituo cha afya kuporwa.
Mashirika hayo matatu yanatoa wito kwa pande zote kwenye mzozo huo kusitisha mara moja mashambulizi dhidi ya misaada ya kibinadamu na kuwalinda raia.