Dar es Salaam. Sherehe za Maadhimisho ya Mwaka Mpya wa Kichina (Chinese New year festival), zilizofanyika jana usiku katika Ubalozi wa China nchini Tanzania zimetumika kama jukwaa muhimu la kidiplomasia katika kuimarisha urafiki wa muda mrefu kati ya Tanzania na China.

Katika hafla hiyo, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, James Millya, alipomwakilisha Waziri wa wizara hiyo Mahmoud Thabit Kombo ambaye hakufika, ameeleza umuhimu na fursa za kuandaa Mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 na kuomba China kuunga mkono juhudi za ujenzi wa miundombinu ya kisasa na yenye sifa za kimataifa.

Tanzania, ikishirikiana na mataifa ya Kenya na Uganda, itakuwa mwenyeji mwenza wa mashindano hayo mwakani.

Millya amesisitiza kuwa maandalizi ya mashindano hayo makubwa ya soka si tu tukio la michezo, bali ni fursa ya kimkakati ya maendeleo ya kiuchumi na kidiplomasia kwa Taifa na ukanda wa Afrika Mashariki.

Raia wa Kichina na Viongozi mbalimbali nchini Tanzania wakishiriki maadhimisho ya Sherehe za mwaka wa kichina (Chinese New year Festival), jijini Dar es Salaam, jana Februari 6, 2026.

Ameeleza kuwaTanzania inahitaji viwanja vya michezo vinavyokidhi viwango vya kimataifa, usafiri na miundombinu ya kijamii inayohusiana na mashindano hayo.

“Kwa kuwa Taifa letu kwa kushirikiana na mataifa jirani tunaandaa Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), maandalizi haya yanahitaji miundombinu ya hali ya juu inayokidhi vigezo vinavyohitajika kimataifa, kwa kuzingatia historia ya ushirikiano wa maendeleo na China, tunaomba China kuendelea kusaidia juhudi hizi ili kuhakikisha miundombinu hii inakamilika kwawati na kwa viwango vinavyotakiwa,” amesema.

Millya ameweka wazi kuwa AFCON 2027 si tu tukio la michezo bali ni jukwaa muhimu la fursa za kiuchumi na maendeleo ya kidiplomasia kwa Taifa na kanda.

Amesema michezo hiyo pia ni fursa muhimu katika kuimarisha miundombinu, kuongeza uwekezaji na kukuza utalii.

Katika ombi hilo, Naibu Waziri huyo amesema ushirikiano wa Tanzania na China, umekuwa fursa muhimu katika ujenzi wa miundombinu bora na ya kisasa yenye ufanisi wa muda mrefu katika miradi ya usafirishaji na huduma za kijamii.

Kwa upande wake, Kaimu Balozi wa China, Wang Yong amesisitiza kuwa Mwaka Mpya wa Kichina ni fursa ya mshikamano na safari ya pamoja kwa China na Tanzania akisema kwa Taifa hilo huu ni  Mwaka wa Farasi kuashiria ujasiri, ari na kasi ya maendeleo.

Ameweka wazi kuwa China inaendelea kusonga mbele kiuchumi, kisiasa na kijamii chini ya uongozi wa Rais Xi Jinping, huku ikiimarisha mchango wake katika utawala bora wa dunia na maendeleo endelevu.

Kaimu Balozi wa China nchini Tanzania, Wang Yong, akizungumza katika sherehe za mwaka wa kichina, jijini Dar es Salaam, jana Februari 6, 2026.

 Yong amebainisha kuwa uhusiano wa China na Tanzania umejengwa juu ya urafiki wa kihistoria na mshikamano wa maendeleo.

Kuhusu ujenzi wa miundombinu, Yong amesema mpango wa ushirikiano huo unajumuisha ujenzi wa miradi mikubwa ya miundombinu ikiwemo ukarabati wa Reli ya TAZARA, China ikiwezesha kwa msaada wa kifedha, kiufundi na mbinu za usimamizi.

 “Wachina waliopo Tanzania wakiwemo wafanyakazi, walimu, wanafunzi na wahamiaji ni  daraja muhimu la mafunzo, ushawishi wa kiuchumi, na kubadilishana maarifa,” amesema.

Naibu Waziri Millya amepongeza na kubainisha kuwa juhudi hizi za ujenzi wa miundombinu zinahusiana moja kwa moja na mpango wa mkakati wa ushirikiano wa kimkakati kati ya Tanzania na China katika kuhakikisha maendeleo ya pamoja.

Amesisitiza kuwa miradi hii itaimarisha uchumi wa Taifa na kikanda, kuendeleza usafirishaji wa bidhaa, kuongeza ajira, na kuboresha huduma za kijamii.

Aidha, Yong amebainisha kuwa uhusiano wa China na Afrika unakua kwa misingi ya mabadilishano ya kijamii na kitamaduni, huku akitilia mkazo kuwa mafanikio ya pamoja na ushirikiano wa kisiasa na kiuchumi ni eneo muhimu katika ushirikiano wa Taifa hilo na mataifa ya Afrika.

 Amesisitiza pia kuwa China itaendelea kushirikiana na Tanzania kuhakikisha utekelezaji wa makubaliano ya  Beijing ya mwaka 2024, yanayolenga kuhakikisha miradi mikubwa inatekelezwa kwa ufanisi na inaleta maendeleo endelevu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *