Tarime. Serikali mkoani Mara imetoa siku 90 kwa mkazi anayeishi jirani na bwawa la kuhifadhi maji yenye sumu (TSF) katika mgodi wa dhahabu wa Barrick North Mara wilayani Tarime kuhama kwa hiari, vinginevyo atalazimishwa kuondolewa kwa nguvu kwa sababu za usalama.
Hatua hiyo inakuja huku zaidi ya wakazi 70 wakigoma kuchukua fidia ili kupisha upanuzi wa shughuli za mgodi, baadhi wakidai kutoridhishwa na viwango vya malipo na kutaka kuongezewa fedha.
Akizungumza leo Februari 28, 2026 alipotembelea eneo hilo, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi alisema baada ya muda uliotolewa kumalizika Serikali itachukua hatua kali kwa atakayesalia katika eneo hatarishi karibu na bwawa la sumu.
“Baada ya siku 90 nisikute mtu hapa, la sivyo tutakuja na greda kubomoa nyumba. Hii ni kwa usalama wake na familia yake, kuishi karibu na bwawa lenye maji ya sumu ni hatari,” amesema.
Pia ameagiza Ofisi ya Mwanasheria wa Serikali mkoani humo kuwasilisha hati ya dharura mahakamani ili kesi inayomhusu mmiliki wa nyumba 44, Ezra Wambura, isikilizwe kwa haraka baada ya mgogoro uliomfanya akatae fidia.
Kanali Mtambi amehoji uhalali wa uwepo wa nyumba 44 ndani ya ekari moja na kuagiza uchunguzi ufanyike kubaini kama taratibu zilifuatwa katika ujenzi wake.
Amesema kugomea fidia kunakwamisha uwekezaji na juhudi za Serikali kuleta maendeleo kupitia sekta ya madini, akisisitiza kuwa mgodi huo una umiliki wa Serikali hivyo manufaa yake ni ya Watanzania.
Awali, Meneja Mahusiano wa Barrick North Mara, Francis Uhadi alisema watu 74 wamegoma kupokea fidia licha ya mazungumzo ya muda mrefu yaliyoshirikisha viongozi wa vijiji.
Amesema baadhi wanataka malipo ya ziada zaidi ya tathmini ya wataalamu, akitoa mfano wa mkazi anayetakiwa kulipwa Sh83 milioni lakini anashinikiza kuongezewa Sh9 milioni.
Kuhusu eneo la Ezra Wambura, Uhadi almesema mgogoro umetokana na mikataba ya awali kati yake na watu waliomjengea nyumba kwenye ardhi yake, hali iliyosababisha mvutano wakati wa ulipaji fidia.
Meneja Mkuu wa mgodi huo, Apolinary Lyambiko amesema kampuni inaendelea kulipa fidia kwa kaya 254 zinazotakiwa kupisha ekari 59 kwa upanuzi wa shimo la Nyabirama, hatua inayolenga kuongeza uzalishaji na kuimarisha usalama.
Amesema baadhi ya walengwa wamechagua kulipwa fedha taslimu, huku wengine wakichagua kujengewa nyumba mbadala; tayari nyumba 10 zimekamilika na nyingine ziko hatua mbalimbali za ujenzi.
Hata hivyo, mmoja wa wakazi waliogoma fidia, Mwita Wiso amedai tathmini ina mapungufu ikiwamo nyumba yake moja kutoingizwa, pamoja na kiwango cha fedha kuwa kidogo kulinganisha na thamani ya ardhi na gharama za ujenzi Nyamongo.
Baada ya maelezo hayo, Mkuu wa Mkoa ameagiza tathmini ya madai hayo ifanyike haraka ili uamuzi uchukuliwe na mkazi huyo aondoke kupisha shughuli za mgodi.