Dar es Salaam. Ni wazi kuwa sanaa ya uchoraji ni moja ya utamaduni wa Kiafrika. Kwani yapo makabila kadhaa Tanzania ambayo huchora michoro mbalimbali kwenye miili yao kama lile la Wamakonde, Wanyamwezi na mengineyo. 

Uchoraji huo uhusisha Makaa ya moto, Mimea na mizizi ama vifaa vya kuchanjia.

Mbali na aina hiyo ya uchoraji. Siyo ajabu kukutana na mwanamke aliyechora hinna kwenye mwili wake. Huku wapo wanaohusisha urembo huo na dini ya Kiislam kwani ni moja kati ya tamaduni ya Kiarabu na hupendelewa katika matukio ya ndoa au mwezi wa Ramadhan. Fahamu zaidi,

Hinna ni rangi ya asili inayotokana na majani ya mmea unaoitwa ‘Lawsonia inermis’.

Majani yake hukaushwa, kusagwa hadi kuwa unga, kisha huchanganywa na maji au majimaji mengine ili kutengeneza rangi inayotumika kupaka au kuchora michoro kwenye ngozi, nywele na kucha.

Michoro ya hinna huwa ya muda mfupi hudumu kwa siku chache hadi wiki kadhaa kabla ya kufifia taratibu. 

Akizungumza na Mwananchi yaliyojificha katika urembo huo sheikh Khamisi Mataka anasema hinna haipaswi kupakwa na kila mwanamke

“Hinna ni moja ya mapambo ya mwanamke, yameandaliwa maalumu kwa ajili ya mume wake ili kumvutia. Hinna inastahili wanawake walioolewa wao ndio wanapaswa kupaka hinna kwa ajili ya kuwapendezesha waume zao.

“Siyo jambo la kuonekana hadharani linahusu mume na mke.  Wanaopaka na kuionesha wazi wanakosea kwa sababu kwa mujibu wa uislamu mwanamke viungo vinavyotakiwa kuonekana wazi ni sura na viganja vya mikono tu,” anasema.

Hata hivyo, wapo baadhi ya wanaume wanaopendelea pambo hilo kupaka kwenye ndevu Mataka anasema hilo siyo kosa.
“Kwenye ndevu imeruhusiwa isipokuwa kuzitia rangi nyeusi. Hapo itakuwa unakataa weupe wa mvi. Faida zake ni pambo tu,” anamaliza Mataka.

Naye Aisha Mpatila, Mwanahabari wa Umoja wa Wanawake wa Kiislamu ‘BAKWATA’ anasema licha ya kuwa pambo hilo ni maalumu kwa ajili ya wanawake walioolewa. Pia wapo wanaopaka kwa kujifurahisha.

“Mtu asiyeolewa anatakiwa achore kwa ajili ya kujifurahisha lakini anatakiwa kuficha isionekane kwani akiona wanaume ni haramu. Lakini kwenye sherehe ya wanawake watupu unaweza kupaka na asijifunike. Akitoka hapo aifiche,”anasema Aisha.

Hata hivyo, kutokana na maendeleo ya teknolojia anasema mtu anaweza kutumia hinna yoyote kwani kwa sasa zipo nyingi.
“Uchore sehemu yenye stara. Mwezi mtukufu watu huchora kwa ajili ya kuufurahia mwezi huo. Lakini nashauri tuwachoree wanaume zetu. 

“Kama hujaolewa usichore hinna utaenda kujitia shida. Sisi mabibi zetu ilikuwa kama hujaolewa marufuku kuchora ilikuwa hadi unapigwa. Turudi kwenye enzi zetu,”anasema Aisha

Mitazamo ya watu

Habiba Said, mtumiaji wa urembo huo kutoka Temeke Dar es Salaam, anasema anapenda kupaka licha ya kuwa mume wake hapendi.

“Napenda kwa sababu mimi ni Mhehe, lakini nimelelewa na Wazanzibar nimekuwa nikiwaona tangu mdogo wanachora piko na hinna kipindi cha Eid. Zamani nyumbani nilikuwa nakatazwa kwa sababu nilikuwa sijaolewa.

“Binafsi nimeanza kuutumia urembo huo katika maandalizi yangu ya kuolewa mwaka 2022. Mimi napenda kuchora lakini mume wangu hapendi, hanikatazi lakini anasema havutiwi na mwanamke anayechora,”anasema

Anasema hilo linamfanya asichore hinna mara kwa mara ili asimkere mume wake. 

Mbali na Habiba, Tatu Ibrahim mkazi jijini humo anasema kwasababu anapenda urembo huo hulazimika kuutumia licha ya kuwa anakosea.

“Napaka kwa sababu ya urembo nikiona watu natamani. Najua ni pambo la mke kwa mume, mimi huwa nachora kwa makosa sababu sijaolewa. 

“Mama yangu huwa ananisema sana. Mara nyingi huwa nachora kwenye Eid na kwenye harusi za ndugu. Kawaida nyekundu ndiyo inanivutia napenda maua makubwa,”anasema Habiba
Naye Hamis Twalib mkazi wa Kondoa anasema Hinna huongeza msisimko zaidi.

“Nikiona mwanamke amepata huwa nafurahia sana, inanipa msisimko zaidi ni kitu ambacho nakipenda. Mke wangu hupendelea kupaka nikiwa nakaribia kurudi safari, kwenye sherehe na mwezi mtukufu,”anasema Hamis.

Akizungumza na Mwananchi Shamira Mkopi mchoraji hinna Tabata, anasema wateja wake ni mchanganyiko.

“Siwezi kusema wateja wangu wote wameolewa hapana. Wapo mchanganyiko kwa sababu siku hizi wengi wanapaka kama urembo tu ingawa ni kweli inatakiwa wapeke walio kwenye ndoa.

“Bei yake hutegemeana na aina ya maua na ukubwa wa eneo analopata. Maua yanaanzia Sh5000 kwenye viganja vya mikono,”anasema.

Akimalizia Halima Misiwa, fundi wa uchoraji hinna anasema wanawake wanaokaribia kuolewa ndio wateja wake wakubwa.

“Wateja wangu ni wale wanaokaribia kuolea, huwa nawachora maeneo mbalimbali kama vile kwenye kiuno, mikono, miguu na maeneo mengine.

“Kuelekea mwezi mtukufu wa Ramadhan nimepokea tenda nyingi sana wote wanataka kupendeza. Urembo wa hinna sio wa kubezwa tuendeleze tamaduni zetu. Unaweza kutumia aina yoyote ya hinna unayotaka,”anasema.
 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *