
Chini ya wiki mbili tu baada ya maporomoko ya ardhi katika mgodi wa madini ya coltan wa Rubaya katika mkoa wa Kivu Kaskazini, janga lingine kama hilo lilitokea mwishoni mwa wiki hii iliyopita nchini DRC, wakati huu katika mgodi wa shaba wa kienyeji wa Tulizembe nje kidogo ya Kolwezi kusini mwa nchi. Wachimbaji madini 12 walifukiwa wakiwa hai wakati mgodi huo uliporomoka.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Na mwandishi wetu huko Lubumbashi, Denise Maheho
Katika miaka miwili tu, wachimbaji madini zaidi ya 20 wamepoteza maisha katika mikasa ya maporomoko ya ardhi katika mgodi wa Tulizembe, eneo ambalo linaajiri takriban wachimbaji madini 10,000 kusini mwa DRC. Kufuatia janga hili la hivi karibuni, mashirika ya kiraia yanadai hatua za usalama kuongezwa katika mgodi huo.
Wakati huu, waathiriwa waliingia mgodini usiku kuchimba shaba kabla ya kujikuta wamenaswa baada ya kuporoka kwa ardhi. Ingawa idadi rasmi iliripoti vifo 11 na majeruhi sita, mchimbaji mmoja wa kumi na mbili baadaye alifariki kutokana na majeraha yake.
Mazingira mabaya ya kazi
Kulingana na Thimothé Mbuya, mkurugenzi wa shirika lisilo la kiserikali la Justicia Asbl, chanzo chake ni mazingira mabaya ya kazi katika eneo hilo. “Mbali na mvua kubwa ambayo imekuwa ikikumba eneo hilo, vyama vya ushirika vya uchimbaji madini vinatumia vifaa bila kuheshimu viwango vya usalama. Matokeo yake, uwezekano wa kujikuta wakikabiliwa ongezeko la matukio mabaya,” anaelezea.
Leonard Zama, mwanaharakati wa haki za binadamu huko Kolwezi, analaani uzembe wa huduma za umma. “Katika wiki chache tu, zaidi ya watu thelathini wamepoteza maisha yao katika eneo la Mulondo, miili mitano imepatikana Kisankala, na wachimbaji 11 wamepoteza maisha huko Tulizembe. Idadi hii ni kubwa mno! Mamlaka inatakiwa kuchukua hatua ili kuhakikisha usalama wa wachimbaji madini kwa kutumia mfumo wa kienyeji,” amesema.
Ingawa tayari imesimamisha shughuli katika eneo la Tulizembe, ambalo ililiona kuwa hatari, Idara ya Usaidizi na Usimamizi wa Uchimbaji Madini kwa kutumia mfumo wa kienyeji inapanga ukaguzi wa maeneo yote ya uchimbaji madini yenye hatari kubwa katika eneo la Kolwezi.