Ikiwa ni katika kuadhimisha mwaka wa 47 wa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, maandamano ya tarehe 22 Bahman sawa na tarehe 11 Februari yamefanyika mjini Tehran sambamba na miji mingine mingi, yakiushirikisha umati mkubwa wa watu katika pembe zote za nchi.
Wananchi katika pembe zote za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran jana Jumatano walifanya matembezi makubwa ya kuadhimisha mwaka wa 47 wa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, ambapo walitangaza upya utiifu wao kwa misimamo ya muasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, na kusisitiza kuendelea kufuata njia ya mashahidi watukufu wa nchi hii hadi ushindi wa mwisho wa Iran dhidi ya maadui zake.
Katika ujumbe aliotoa kwa mnasaba huu kwa njia ya televisheni, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aliitaja tarehe 22 Bahman kuwa siku ya kudhihirisha nguvu na adhama ya taifa la Iran na kusisitiza kwamba, kushiriki kwa wingi wananchi katika maandamano haya na kutangaza upya utiifu wao kwa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu kutamfanya adui arejee nyuma na kutokuwa na tamaa na Iran pamoja na maslahi yake ya kitaifa.
Bahman 22 ni ukumbusho wa moja ya matukio makubwa ya kihistoria ya taifa kubwa la Iran ambapo wananchi wanamapinduzi wa Iran humiminika mitaani kila mwaka na katika kila mazingira kwa ajili ya kuwathibitishia walimwengu umoja na mshikamano wao katika kulinda thamani na malengo matukufu ya Mapinduzi ya Kiislamu.
Ushiriki wa wananchi katika matembezi ya tarehe 22 Bahman ni uwanja wa kudhihirishwa mwamko, umakini, umoja, mshikamano na uzingatiaji wao wa hatima ya nchi na tangazo la kuchukizwa kwao na maadui wa mfumo wa Kiislamu, jambo ambalo linatoa pia bishara njema kwa marafiki wa mfumo wa Kiislamu na wakati huo huo kuzima njama za maadui wa ndani na nje wa Mapinduzi ya Kiislamu.

Kama moja ya hafla muhimu za kisiasa na kijamii nchini, maandamano ya Bahman 22 ni kiakisi cha umoja wa kitaifa, uaminifu kwa malengo ya Mapinduzi ya Kiislamu na ishara ya nguvu ya watu wa Iran.
Mapinduzi ya Kiislamu yamekuwa na nafasi muhimu si tu kwa watu wa Iran na Waislamu wa nchi nyingine, bali pia yamekuwa kigezo muhimu kwa watu wanaopigania uhuru na kujitawala katika pembe mbalimbali za dunia. Kwa hivyo, matembezi makubwa ya tarehe 22 Bahman yanachukuliwa kama ukumbusho wa maadili, malengo matukufu ya Mapinduzi na ustaarabu wa kisasa wa Kiislamu kwa Waislamu na wapenda-uhuru wote ulimwenguni.
Uwepo huu ni ishara ya uthabiti wa kisiasa na uungaji mkono wa wananchi kwa mfumo wa Kiislamu, jambo linalozingatiwa pia katika ngazi za kimataifa. Mahudhurio ya watu wengi katika maandamano ya Bahman 22 bila shaka yanapunguza njama za vyombo vya habari vya kigeni za kuchochea migawanyiko na kuwakatisha tamaa watu wa Iran.
Maandamano ya tarehe 22 Bahman pia ni ishara ya kitamaduni ya uwepo wa vizazi vipya na kufahamiana kwao na maadili ya Mapinduzi ya Kiislamu. Mshikamano wa kitaifa, uthabiti na sisitizo la kuunga mkono malengo matukufu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni miongoni mwa madhihirisho muhimu zaidi ya kitamaduni ya tukio hili kubwa nchini.
Maandamano ya tarehe 22 Bahman yenye kauli mbiu za kupinga ubeberu na dhulma ni mfano wa kuigwa na mataifa mengine ya dunia hasa ya eneo la Asia Magharibi.
Kwa hiyo, ujumbe wa Iran kama kitovu cha muqawama na kujitawala, unaimarika zaidi na uhalali wake wa kimaanawi kuongezeka katika ulimwengu wa Kiislamu.
Maandamano ya tarehe 22 Bahman ni ishara ya nguvu na uhai wa Mapinduzi ya Kiislamu, uwepo ambao si tu kwamba unakumbusha maadili thabiti ya Mapinduzi, bali pia unadhamini mustakabali imara wa taifa.
Usalama wa taifa unaodhaminiwa na uwepo mkubwa wa watu wa Iran uwanjani ndilo suala muhimu zaidi kwa nchi, ambapo maadui hujiepusha kuchukua hatua zozote za uhasama dhidi ya taifa kama hili lenye umoja na mshikamano.
Maandamano ya kila mwaka ya tarehe 22 Bahman ni ishara ya mshikamano wa kweli wa taifa la Iran, mshikamano uliokita mizizi katika imani, utambulisho wa kitaifa, uaminifu kwa Mapinduzi ya Kiislamu na kutetea uhuru wa nchi. Kushiriki kwa wingi watu katika siku hii kunaonyesha kuwa taifa la Iran lina umoja wa kistratijia katika kukabiliana na vitisho na uadui wa kigeni dhidi ya mfumo wake.