- Baraza la Magavana (CoG) limeapa kususia wito wa Kamati ya Seneti ya Hesabu za Umma za Kaunti (CPAC), likiwashutumu baadhi ya maseneta kwa madai ya ulaghai wa fedha, unyanyasaji na misako ya kisiasa
- Magavana wamewataja Moses Kajwang, Edwin Sifuna, Samson Cherargei na Johnes Mwaruma kuwa miongoni mwa wanaojihusisha mara kwa mara na vitisho, wakitaka waondolewe kwenye kamati za uangalizi
- Huku wakisisitiza kujitolea kwao kwa uwajibikaji, magavana wanasema uangalizi lazima uwe wa kisheria na wa kimaadili, na wametaka kuwe na ushirikiano wa kimuundo na uongozi wa Seneti kutatua mvutano huo
Baraza la Magavana (CoG) limesisitiza msimamo wake wa kupinga wito wa Kamati ya Seneti ya Hesabu za Umma za Kaunti kufuatia madai ya ulaghai na unyanyasaji.

Source: Twitter
Magavana waliwataja wajumbe wanne waandamizi wa kamati hiyo kuhusika katika madai ya ulaghai.
Katika taarifa kwa vyombo vya habari, baraza hilo liliwatuhumu maseneta Moses Kajwang wa Homa Bay, ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati, Edwin Sifuna wa Nairobi, Samson Cherargei wa Nandi na Johnes Mwaruma wa Taita Taveta kwa kuendeleza unyanyasaji na ulaghai.

Pia soma
Magazeti ya Kenya, Februari 11: Njama ya kumtimua Edwin Sifuna ODM yaiva, timu ya Oburu yakutana
“Tunatambua kwa wasiwasi mkubwa taarifa na matukio yanayoendelea ya ulaghai, misako ya kisiasa, vitisho na unyanyasaji wa magavana wakati wa kuhojiwa mbele ya Kamati ya Seneti ya Hesabu za Umma za Kaunti (CPAC). Ili kuondoa shaka yoyote, tunawasilisha kwamba maseneta wafuatao wametajwa mara kwa mara kuwa wahusika wakuu wa vitendo hivi: Moses Kajwang, Edwin Sifuna, Samson Cherargei na Johnes Mwaruma,” baraza hilo lilisema.
Magavana waliapa kususia wito wa kamati hiyo hadi masuala waliyoyaibua dhidi ya maseneta hao yashughulikiwe.
Wakati huo huo, walitaka kuondolewa kwa maseneta hao kutoka kamati za Seneti ili kurejesha imani, uadilifu na haki katika mchakato wa uangalizi.
Magavana hao, huku wakieleza kujitolea kwao kikamilifu kwa uwajibikaji na matumizi bora ya rasilimali za umma, waliomba kufanyika kwa mkutano wa pamoja na Seneti ili kutatua masuala wanayodai ni vikwazo kwa mchakato wa uwajibikaji.
Hapo awali wakuu hao wa kaunti walikuwa wameonya kuwa wangesusia vikao vya kamati hiyo lakini hawakuwa wamebainisha maseneta waliokuwa na matatizo nao.
Mwenyekiti wa CoG na Gavana wa Wajir, Ahmed Abdullahi, akizungumza baada ya warsha Kilifi, alieleza wasiwasi kuhusu kile alichokitaja kama kuongezeka kwa ulaghai, misako ya kisiasa, unyanyasaji, vitisho na udhalilishaji wa magavana.
Alisema baraza limeamua kutofika mbele ya kamati hiyo hadi malalamishi yao yashughulikiwe kupitia ushirikiano wa kimuundo na uongozi wa Seneti.
Abdullahi alieleza zaidi kuwa magavana huitwa mara kwa mara mbele ya Kamati ya Seneti ya Uwekezaji wa Kaunti na Fedha Maalum kujadili uwekezaji katika manispaa, hospitali na kampuni za maji.
Walikubaliana kufika mara moja tu kwa kila mzunguko wa ukaguzi wa hesabu.
Alisisitiza kuwa ingawa baraza linaendelea kujitolea kwa uwajibikaji, uangalizi lazima uwe wa kisheria, wa kimaadili na usio na matumizi mabaya ya mamlaka.
Seneta Kajwang alitupilia mbali msimamo wa magavana, akisema unafanana na kutoa masharti kwa Seneti.
Alirejelea ripoti za Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na taarifa za vyombo vya habari kuhusu madai ya wizi wa rasilimali za kaunti, akibainisha kuwa Ibara za 229 na 125 za Katiba zinampa Seneti mamlaka ya kupitia ripoti hizo na kuita mashahidi.
Read ENGLISH VERSION
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia news@tuko.co.ke au WhatsApp: 0732482690.
Chanzo: TUKO.co.ke
