s

Chanzo cha picha, Sifuna

    • Author, Asha Juma
    • Nafasi, BBC Nairobi
    • Akiripoti kutoka, Nairobi
  • Muda wa kusoma: Dakika 7

Migogoro ya kisiasa ndani ya chama cha Orange Democratic Movement (ODM) nchini Kenya ina maana kubwa kwa siasa za nchi hiyo. Kuna msemo usemao, “mti mkuu ukianguka ndege huwa mashakani,” na kwa wanaofuatilia siasa za Kenya, msemo huu unaonekana kupata uzito wake hasa baada ya kuondokewa na kinara wa chama hicho, Raila Odinga.

ODM si tu kwamba kinatambulika nchini Kenya pekee, bali pia kimejijengea jina kama chama chenye ushawishi mkubwa katika siasa za Afrika Mashariki na hata kimataifa.

Kwa zaidi ya miaka ishirini tangu kuanzishwa kwake mwaka 2005, chama hiki kimekuwa nguzo muhimu ya siasa za Kenya. Nguvu yake ilidhihirika wazi wakati wa kura ya maoni ya katiba mwaka 2005, ambapo kilipinga rasimu iliyopendekezwa na msimamo wake ukaungwa mkono na wananchi hadi kura ya ‘Hapana’ ikashinda na katiba hiyo kutopitishwa.

Vilevile, mwaka 2010, ODM chini ya uongozi wa Raila Odinga ilipoongoza kampeni ya kura ya ‘Ndio’, katiba mpya ilipitishwa. Haya yote yanaonyesha jinsi chama hicho kilivyokuwa na ushawishi mkubwa katika maamuzi ya kitaifa.

Leo, chama hicho hicho kinakabiliwa na changamoto za migawanyiko ya ndani, jambo linalozua maswali kuhusu mustakabali wake katika enzi mpya baada ya kiongozi wake mkuu kuondoka, lakini pia migogoro hiyo inaanza kutikisa siasa za Kenya.

Kutimuliwa kwa Katibu Mkuu wa ODM

S

Chanzo cha picha, SIFUNA

Chungwa lililokuwa tamu na kukata kiu ya wengi waliokuwa wanafungamana nalo kisera, leo limegeuka kuwa chungu kwao. Tuanze na tukio la hivi karibu zaidi, Edwin Sifuna, Katibu Mkuu wa ODM ametimuliwa chamani.

Baraza Kuu la chama hicho kikuu cha upinzani kilichukua uamuzi huo na kupitia Naibu Katibu Mkuu Catherine Omanyo, kilizungumzia ukosefu wa nidhamu katika ngazi ya uongozi na kuongeza kuwa ODM inaongozwa na katiba yake.

”Baada ya kujadiliana juu ya masuala yenye kuhusiana na mienendo ya Katibu Mkuu, Seneta Sifuna, Baraza la chama limeamua kumvua majukumu yake mara moja, kulingana na katiba ya chama na sheria,” Omanyo alisema wakati wa mkutano na wanahabari.

Sifuna amejitokeza hadharani mara kadhaa akionekana kutengana na misimamo ya sasa ya chama cha ODM ambayo ni pamoja na kuunga mkono serikali inayoongozwa na chama cha UDA.

”Ameonekana katika mikutano akisema, ‘Baba hakulea watu waoga, na Baba alikuwa anatuambia kila siku, Sifuna chunga maslahi ya mwananchi,” Sifuna alisema katika mkutano wa kisiasa’.

Matamshi kama hayo na mengine huenda ndio yaliyomchongea Sifuna kiasi cha kutemwa nje. Lakini nini hasa kinasababisha migawanyiko ndani ya ODM ambayo imekuwa ikionekana kila pembe?

Chachu ya kifo cha polepole cha ODM

AS

Chanzo cha picha, AFP

Uchu wa madaraka ni jambo ambalo lilijitokeza ndani ya chama hata kabla ya Raila Odinga kuaga dunia. Oktoba 2024, gavana wa Kisumu Peter Anyang’ Ngong’o alichaguliwa kuwa kiongozi wa muda wa ODM, hatua mbayo ilisababisha kuzuka kwa maswali mengi kutoka kwa uongozi juu ya msimamo na umri wake. Hii ilikuwa ni dalili ya mawingi, iliokuwa inajaribu kuashiria kwamba chama kisipokuwa makini kuna wakati mvua ya migogoro itawanyeshea na kama kweli, sasa imeanza kumwaika.

Baada ya Odinga kufariki dunia, Oburu Odinga kaka yake Raila Odinga ndiye aliyepewa jukumu la kuongoza chama cha ODM kwa muda lakini muda si muda, wanachama kama kina Sifuna walianza kuhoji uhalali wake wa kuteuliwa katika wadhifa huo.

Akizungumza katika Runinga ya Citizen, Sifuna alidai kuwa uteuzi wa Oburu Odinga, ambaye ni kaka mkubwa wa marehemu Odinga, ulikuwa na dosari za kiutaratibu na ulipuuzwa na kanuni za chama zilizowekwa.

“Kuteuliwa kwa Oburu Oginga kama kiongozi wa muda wa chama hakukufuata utaratibu kulingana na vipengee vya Katiba,” Sifuna alisema.

Mgawanyiko huu umeendelea hasa lilipokuja suala la chama cha ODM kuunga mkono chama cha UDA, ambako hadi Odinga anafariki dunia kilionekana kuwa pamoja na serikali ya Rais Ruto.

Baada tu ya ‘Baba’ kuzikwa, wanachama waliokuwa na mawazo tofauti na kujiunga na UDA walionekana kujitenga, na kujigawa ndani ya ODM kukajitokeza tena.

Wanachama kama mwanasiasa mkongwe James Orengo alisema chama cha ‘ODM hakiwezi kujiunga na UDA’, mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino na mwana wa Raila Odinga Winnie Odinga wakionekana kumuunga mkono Sifuna huku kambi iliyotaka kuendelea kuwa kwenye serikali ikimuunga mkono Oburu Odinga aliendelea kukumbatia ODM kuachwa ndani ya serikali ya Ruto.

Ubabe na fahari pia vinauwa ODM taratibu. Chama kawaida hakiwezi kuundwa bila miongozo ambayo hutumika kutoa mwelekeo wa chama katika kila hatua. Lakini hali chamani inakuwa ngumu wakati kila mmoja anataka kuonyesha ubabe na nguvu yake ya kisiasa. Tuchukulie mfano wa maisha ya nyumbani, lazima kuwe na kichwa na shingo ndio mambo yaweze kwenda kwa uzuri na pale kila mmoja atakapotaka kuwa kichwa, hata majirani watajua kuna shida mahali.

Tukubali kuwa kila mmoja anaushawishi katika ngome yake na umuhimu katika chama lakini umoja ukikosekana ndio pale panaposhuhudiwa mgogoro kama huu wa sasa ndani ya ODM.

Kuwa na mawazo tofauti ni jambo la kawaida sana lakini haimaanishi kuwa sasa, hilo liwe chanzo cha ODM kujigawanya makundi na kulikata chungwa vipande vipande.

Athari za migogoro ya ndani ya ODM

s

Chanzo cha picha, Getty Images

Kufukuzwa kwa Sifuna chamani kuna maanisha nini? Mchambuzi wa siasa nchini Kenya Dkt. Martin Oloo amezungumza na BBC na kusema kuwa uamuzi iliochukuliwa na ODM wa kumvua Sifuna cheo cha Katibu wa chama sio wa busara kwa sababu Sifuna amejiweka kama mtetezi wa vijana na pia ana wafuasi wake.

”Ni kosa kubwa kwao kumfurusha na bila shaka ni kumpa umaarufu,” Oloo alisema.

Ifahamike kuwa Sifuna alikuwa na wafuasi wake na kufikia sasa, hakukosekani wale ambao tayari wameshaamua kumfuata unyo unyo, wasiburu tu kujionea ni wapi kiongozi wao anapoelekea. Na kama haitoshi, ndani ya chama kuna wale waliokuwa naye kwenye kambi moja. Ni hatua gani watakayochukua wakati mmoja wao tayari ameonyeshwa mlango? Kadiri muda unavyokwenda, fumbo hili pia nalo litapata ufumbuzi.

Kupungua kwa ushawishi wa chama

Wakati sarakasi za ndani ya chama cha ODM zinaendelea, hatari ya chama kuyumba zinaongezeka jambo ambalo linapunguza uimara wake kisiasa.

Nguvu ya chama cha ODM ndio imekuwa silaha kubwa ya kuweza kuingia ndani ya serikali pale iliposemekana kuwa chama hicho kimeshindwa katika uchaguzi mkuu.

Kwa mfano, marehemu Raila Odinga alifanikiwa kuwa Waziri Mkuu wa Kenya baada ya uchaguzi wa mwaka 2008. Hii ni kwa sababu ya uzito aliokuwa nao kisiasa na uimara wa chama chake vyingine, pengine ingekuwa vigumu kwa jambo kama hilo kutokea.

Sasa kwa kasi ambayo chama cha ODM kinaporomoka tena kutokana na mgawanyiko wa ndani, suali ni je, siku zijazo, kitakuwa na sauti gani ya kuweza kujitetea kabla ya kutetea wananchi kama ambavyo wafuasi wake walikuwa wamezoea.

Hatari ya kujitoa katika chama

s

Chanzo cha picha, Getty Images

Kwa jinsi hali ilivyo, ni wazi kuwa kuendelea kwa mizozo na migawanyiko, kuna uwezekano mkubwa wa chama cha ODM kuendelea kusambaratika na kugawanyika. Matokeo yake, kuna kambi ambazo zinaweza kujiunga na yule ambaye wakati fulani alionekana kuwa adui. Hatua kama hii inaweza kuwa changamoto kwa ODM kujistawisha na kurejea kwa ulingo wake wakati tayari chungwa limeshaingia hila.

Athari katika siasa za Kenya kwa ujumla

ODM kwa wengine ilikuwa ni chama cha kuwawezesha kupanda kwenye majukwaa ya kisiasa lakini ukitathmini kwa undani, ni zaidi ya chama tu hasa ukiangalia uzito wake.

Hii ni sehemu ambayo wananchi wangehisi kutengwa kutokana na maamuzi ya jambo fulani au hatua fulani iliyochukuliwa na serikali, kama chama kikuu cha upinzani wafuasi hao au hata raia kwa ujumla walikuwa na mahali pa kukimbilia na kusemama tutapata mtetezi.

Lakini migogoro ya ndani ya chama inafanya iwe vigumu kwa ODM kuhakikisha uwajibikaji wa demokrasia unatekelezwa katika kila hatua.

Chama kikiwa kinayumba, kuna uwezekano wa kukosa hata nguvu ya kuhoji kwa ujasiri yale yanayotendeka ambayo ni kinyume na matakwa ya wananchi au hata katiba.

Kupungua kwa imani ya wapiga kura

s

Chanzo cha picha, Getty Images

Kuna watu ambao pengine katika maisha yao yote hawajawahi kupigia kura chama kingine zaidi ya kile alichokuwa na imani nacho. Ila malumbano ya kisiasa yakianza kujitokeza hadharani kiasi cha wapiga kura kushindwa ni njia gani watakayofuata, imani yao katika chama inapungua. Kama mzaha, huu unaweza kutambukia usaha na kuwa mwisho wa chama. Bila kujua, wakikizika kwa mikono yao wenyewe na kukitia kwenye kaburi la sahau kwa sababu chama ni watu na watu ni chama.

Hakika, kama nilivyogusia wakati ninaanza, mambo yakuzungumzia ni mengi lakini muda nao unaendelea kutupa kisogo. Miaka ya nyuma ingekuwa vigumu kufikiria kuwa, chama ambacho kimekuwa na umaarufu na msisimko wa aina yake kwa miaka 20, kingeweza kutikiswa kiasi hiki ndani ya miezi michache tu.

ODM ina kazi kubwa ya kufanya kuhakikisha inaendelea kusalia na umuhimu wake na ushindani uliovutia wengi.

Pia kuna fursa ya kuboresha demokrasia ya ndani ya chama hasa kwa kukumbatia mazungumzo ya uwazi, uongozi stahiki na mipangilio muruwa inayoongozwa na sera madhubuti jambo ambalo hamna shaka, limekuwepo pengine tu lilitatizika na migogoro kidogo ambayo kama ingetatuliwa kwa busara, ODM ya leo ingekuwa na nguvu hata kuliko ya jana.

Kwa sasa nikusubiri na kuangalia ikiwa mivutano ya sasa ni ya kupita au ndio utakuwa mwanzo wa ODM itakayo kuwa ikisimuliwa tu kwa vizazi vijavyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *