Shirika la Utangazaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran (IRIB) limetuma kwa mafanikio satelaiti yake ya kwanza maalumu kwa utangazaji, iitwayo “Jam‑e Jam 1”, inayojulikana kimataifa kama “Iran DBS”. Hatua hiyo inaashiria ngazi mpya ya kimkakati katika kuimarisha miundombinu ya vyombo vya habari vya Iran kupitia anga za juu.

Satelaiti hiyo, inayomilikiwa kikamilifu IRIB, ilirushwa kuekelea anga za mbali kutoka Kituo cha Anga cha Baikonur nchini Kazakhstan.

Jam‑e Jam 1 iliwekwa kwenye obiti dakika chache baada ya kurushwa kwa kutumia roketa ya Proton‑M.

Kwa mujibu wa Idara ya Maendeleo ya Vyombo vya Habari na Teknolojia ya IRIB, Jam‑e Jam 1 ni hatua ya kwanza ya kiufundi na kiutendaji kuelekea utekelezaji wa teknolojia ya kizazi kipya ya redio na televisheni shirikishi (interactive broadcasting).

Satelaiti hiyo imeundwa kwa ajili ya kusambaza mawimbi ya sauti na picha yanayoshirikiana (interactive) kwenda vituo vya utangazaji katika nchi kavu, na hivyo kuweka msingi wa huduma za utangazaji wa umma zilizo shirikishi.

Kwa mujibu wa ratiba iliyopangwa, Jam‑e Jam 1 itahamishwa na kutulia katika nafasi yake ya mwisho ya obiti katika nyuzi 34 Mashariki ndani ya kipindi cha chini ya wiki tatu. Nafasi hiyo ya obiti inatarajiwa kutoa eneo bora la kukidhi mahitaji ya mawasiliano ya IRIB.

Maafisa wamesisitiza kuwa Jam‑e Jam 1 ni satelaiti yenye mwelekeo wa matumizi mahsusi. Tofauti na satelaiti za utangazaji wa moja kwa moja majumbani (DTH), mawimbi yake yanahitaji vifaa vya kitaalamu na maalumu na hayawezi kupokelewa kwa kutumia ‘dish’ au sahani ya satelaiti ya kawaida ya nyumbani.

Mradi huu unahakikisha miundombinu muhimu ya mawasiliano kwa ajili ya kuimarisha teknolojia ya utangazaji shirikishi ndani ya Shirika la Utangazaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, na unafungua ukurasa mpya wa kile kilichoelezwa kama uhuru wa kiufundi wa vyombo vya habari vya Iran katika nyanja ya utangazaji wa anga za juu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *