Rais wa Kenya William Ruto ametangaza kuwa Kenya itafungua tena mpaka wake na Somalia mwezi Aprili, baada ya kufungwa kwa muda wa miaka 15 kufuatia mashambulizi ya mara kwa mara ya kigaidi. Hatua hiyo inaashiria jaribio jipya la kurejesha harakati za mpakani na kuimarisha ushirikiano wa kikanda.

Mpaka huo ulifungwa rasmi mwezi Oktoba 2011 baada ya mashambulizi kadhaa ndani ya ardhi ya Kenya yaliyotekelezwa na kundi la kigaidi la al‑Shabab, ambalo kwa zaidi ya miaka 15 limekuwa likipigana na serikali ya kati ya Somalia mjini Mogadishu.

Ruto ameandika kwenye mtandao wa X siku ya Alhamisi kwamba:“Haikubaliki kwamba Wakenya wenzetu wa Mandera waendelee kutengwa na jamaa na majirani zao wa Somalia kwa sababu ya kufungwa kwa muda mrefu kwa Kituo cha Mpaka cha Mandera.” Ruto ambaye siku za karibuni ametembelea majimbo yanayopakana na Somalia amesema: “Tutafungua tena kituo cha mpaka mwezi Aprili.”

Mnamo Mei 2023, Kenya na Somalia zilikubaliana kuhusu ufunguzi wa mpaka kwa awamu. Hata hivyo, miezi miwili baadaye, Kenya ilibatilisha uamuzi huo kufuatia kuuawa kwa raia watano na askari polisi wanane karibu na mpaka, katika mashambulizi yaliyotekelezwa na kundi la al‑Shabab.

Mwaka mmoja kabla ya hapo, mipango kama hiyo ya kufungua tena mpaka ilitangazwa wakati wa mazungumzo kati ya aliyekuwa Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta na Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud, lakini haikuwahi kutekelezwa.

Kenya ni mchangiaji mkubwa wa wanajeshi katika operesheni ya kijeshi ya Umoja wa Afrika (AU) dhidi ya magaidi wa al‑Shabab, ambao wanahusishwa na mtandao wa al‑Qaida.

Kenya na Somalia zinashiriki mpaka wa nchi kavu wa kilomita 680, na kwa miaka kadhaa zimekuwa katika mzozo wa kidiplomasia kuhusu eneo la Bahari ya Hindi linalodaiwa kuwa na akiba kubwa ya mafuta na gesi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *