Iran imelaani vikali uamuzi wa hivi karibuni wa utawala wa Israel wa kunyakua ardhi zaidi za Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu, ikisema kuwa hatua hiyo inalenga kupanua “ujenzi haramu wa vitongoji vya walowezi za Kizayuni” na kuimarisha ukaliaji mabavu na hatua kali za kiusalama dhidi ya Wapalestina na kuendelea “mauaji ya kimbari” huko Gaza.

Esmail Baqaei Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameashiria kuendelea kuuliwa Wapalestina katika Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na “ukiukwaji wa wazi wa haki za binadamu na sheria za kibinadamu,” ikiwa ni pamoja na “kuendelea kuwekwa kizuizini kinyume cha sheria Wapalestina katika magereza ya Israel na kuteswa vikali wafungwa wa Kipalestina.”

Baqaei ametaja vitendo hivyo vya Israel kuwa ni vya kijinai vinavyofanywa sambamba na sera ya “mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina na kutokomezwa Palestina kwa njia ya ukoloni. Ametilia mkazo  jukumu la pamoja la serikali zote la kuzuia kuendelea kwa mauaji ya kimbari ya watu wa Palestina na kuzidi kunyakuliwa ardhi zao.

Baqaei amesema kuwa kutoadhibiwa utawala wa Israel kuendelea uungaji mkono mkubwa wa Marekani na baadhi ya nchi za Ulaya kwa utawala huo hasa Ujerumani na Uingereza ni sababu zinazouitia kiburi utawala wa Tel Aviv cha kuendeleza mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina. 

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amekosoa vikali kutochukua hatua Umoja wa Mataifa na vyombo vingine vya kimataifa mkabala wa sera za kikoloni na kujitanua za utawala wa Israel. 

Esmail Baqaei amesisitiza kuhusu msimamo mkuu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kuunga mkono kurejeshwa haki halali za wananchi wa Palestina khususan hali ya kujiamulia mustakbali wao, kujikomboa kutoka katika makucha ya utawala ghasibu na kuasisi nchi yao huru ya Palestina mji wake mkuu ukiwa Quds Tukufu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *