OSLO, NORWAY: Mapambano hayo yanahususisha matumizi ya mbinu zote halali na zilizowekwa kwa mujibu wa katiba na sheria ili kufanikiwa azima ya kujiletea maendeleo na kuinua uchumi wa watu wake.
Norway ni mojawapo ya nchi zilizokuwa maskini sana duniani hadi miaka ya 1960 lakini ugunduzi wa raslimali ya mafuta umebadilisha kabisa taswira ya nchi hiyo na kuwa miongoni mwa mataifa yaliyoendelea.
Nikiwa hapa nchini Norway nimepata fursa ya kufanya mazungumzo na Profesa Kristin Skare Orgeret, Mhadhiri Mwandamizi kutoka idara ya uandishi wa habari katika Chuo Kikuu cha Oslo Metropolitan ambapo ametoa uzoefu wa nchi ya Norway na namna raslimali ya mafuta ilivyosaidia kubadili taswira ya nchi hiyo katika nyanja ya uchumi, elimu na miundombinu.
“Afrika ina raslimali nyingi zinazoweza kusaidia maendeleo yake, nadhani wanapaswa kuzitumia kikamilifu na huo ni wajibu wa viongozi na watunga sera wote kwa ujumla kutunga sera na sheria nzuri ili raslimali za Afrika ziwanufaishe waafrika na si kampuni binafsi au matajiri. Ni lazima serikali iwe na nguvu katika usimamizi wa raslimali.“
Profesa Kristin ambaye amebobea katika masuala ya habari kuhusu mizozo na usalama wa waandishi wa habari ameelezea uzoefu wa Norway katika kusimamia sekta ya mafuta, raslimali pekee iliyobadili uchumi wa taifa hili lililopo kaskazini mwa bara la Ulaya.
Ugunduzi wa mafuta Norway
Profesa Kristin amesema ugunduzi wa mafuta nchini Norway miaka ya 1960 ulibadilisha kabisa historia ya nchi hiyo kutoka kuwa nchi maskini iliyotegemea uvuvi na kilimo kama shughuli kuu ya kiuchumi.
“Mafuta imekuwa bidhaa ya nchi na kikubwa serikali ilifanya ni kumiliki sekta hiyo kwa asilimia 100 na si kuachia kampuni binafsi na imeisaidia sana nchi hii.
Mafuta na maendeleo
Profesa Kristin amesema ugunduzi wa mafuta umechangia pakubwa katika maendeleo ya nchi hiyo na kuifanya kuacha kutegemea sekta moja ya kilimo katika maendeleo yake.
“Mafuta yamefanya Norway iwe nchi tajiri. Raslimali hii imechangia kuendelea mfumo wa elimu, mfumo wa afya ambao ni bure na pia imesaidia wananchi kuzifikia huduma za umma kwa urahisi”
Akizungumzia mtazamo wa raia wa Norway ikiwa wananufaika na raslimali ya mafuta au la Profesa Kristin amesema wapo raia ambao wana mtazamo hasi na wapo wenye mtazamo chanya kuhusu namna raslimali hiyo inavyowanufaisha wananchi moja kwa moja.
SOMA: Manufaa lukuki utafiti wa mafuta, gesi Bonde la Eyasi Wembere
“Wakati raslimali hii inagunduliwa idadi ya wanorway ilikuwa milioni 3 hivi lakini sasa tupo milioni 5 kuelekea milioni 6. Upo wasiwasi ikiwa raslimali hii itanufaisha vizazi vijavyo vya nchi hii.
Aidha Profesa Kristin amesema wanasayansi wa mazingira pia wamekuwa wakipaza sauti kuitaka Norway kuacha matumizi ya nishati hii kwa sababu ya uharibifu wa mazingira.
Ulinzi wa rasilimali ya mafuta
Akizungumzia mtazamo wa raia wa Norway ikiwa wana Imani na namna serikali inavyolinda mapato yatokanayo na mafuta Profesa Kristin amesema kumekuwa na mtazamo nchini humo ikiwa serikali itumie fedha za mafuta kikamilifu au ihifadhi kwa matumizi ya baadaye.
“Raia wa Norway wana Imani na serikali kwa namna ilivyosimamia raslimali hii hata hivyo kuna mijadala mingi kuhusu hatima ya baadaye ya raslimali hii ambayo si ya kudumu lakini watu wanaona matokeo ya uwepo wa raslimali hii.”
Tanzania
Hivi karibuni nchini Tanzania kumekuwa na mjadala kuhusu uamuzi wa serikali kuuza akiba yake ya dhahabu iliyopo Benki Kuu ya Tanzania BOT ili kugharamia miradi mbalimbali ambayo inajengwa kila pembe ya nchi lakini wapo watu waliojitokeza kupinga uamuzi huo.
Ikumbukwe serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan mwaka 2023 ilianza kununua dhahabu na kuhifadhi benki kuu, uamuzi ambao ulichukuliwa mahususi ili kuiwezesha nchi kupata fedha za kigeni kwa ajili ya shughuli mbalimbali za maendeleo.
Aidha katika kipindi cha miaka 10 iliyopita serikali ya Tanzania imejenga na kuanzisha miradi mbalimbali ya kimkakati ikiwemo reli ya kisasa SGR kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza, bwawa la kuzalisha umeme la Julius Nyerere, daraja la JP Magufuli na miradi mingine chungu nzima.
Mchambuzi wa siasa na diplomasia Hamdoun Marcel akizungumza name kwa njia ya simu amesema kinachopaswa kuzingatiwa ni matumizi sahihi ya fedha zitakazopatikana.
“Mwalimu (Nyerere) alisema kila nchi inapaswa kutumia raslimali zake kikamilifu, sasa nongwa iko wapi kwa serikali kutumia akiba yake ya dhahabu kupata fedha ili kugharamia maendeleo?“ Amehoji Marcel na kusisitiza ni wajibu wa kila mwenye mamlaka kuhakikisha fedha zitakazopatikana zinafanya kazi ilisyokusudiwa.
Saidha Hamdoun amesisitiza haja ya mataifa ya Afrika kukuza uwezo wake wa kiuchumi kwa kutumia raslimali kama madini, mafuta, gesi na sekta ya utalii hatua ambayo amesema itachangia nchi hizo kuachana kabisa na utegemezi kutoka kwa wahisani.
Baadhi ya mataifa ya Afrika ambayo yana raslimali lukuki na ambazo bado zinatajwa kuwa hazijabadili kikamilifu maisha ya watu wake ni Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo DRC, Zambia, Angola, Nigeria, Niger na Zimbabwe.
Mwandishi wa makala haya ni mtumishi wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC). Kwa sasa Fredrick Nwaka yuko nchini Norway kwa ajili ya mafunzo ya muda mfupi ya uandishi wa habari.
