
Maelfu ya raia wa Uingereza wamehudumu katika jeshi la Israel wakati wa vita vya mauaji ya halaiki vya utawala huo wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza.
Ripoti iliyochapishwa na ‘Declassified UK’ imefichua kwamba, zaidi ya raia 2,000 wa Uingereza walipigana pamoja na vikosi vya utawala wa Israel wakati wa vita hivyo vya mauaji ya kimbari huko Gaza.
Ripoti hiyo inategemea data iliyopatikana kwa mara ya kwanza kupitia ombi la taasisi ya ‘Uhuru wa Habari’ lililowasilishwa kwa mamlaka za utawala wa Israel.
Takwimu hizo zilizoashiriwa katika ripoti ya hivi karibuni zilijumuisha wanajeshi wa Israel wenye uraia pacha au kadhaa, wanaopigana kwa niaba ya utawala wa Tel Aviv.
Washauri wa masuala ya kisheria waliiambia ‘Declassified UK’ kwamba, takwimu hizo mpya ziliibua wasiwasi mkubwa.
Data hiyo ilifichua kwamba, watu 1,686 wenye uraia pacha wa Uingereza na Israel waliandikishwa jeshini, pamoja na watu wengine 383 waliokuwa na uraia wa madola hayo mawili, pamoja na uraia mmoja wa ziada, na kuwaweka ndani ya kundi kubwa la wanajeshi wa Israel zaidi ya 50,000 wenye uraia kadhaa.
Ripoti hiyo ya Declassified UK ni sehemu ya mashinikizo ya kisheria kutoka kwa vikundi vya kiraia na utetezi nchini Uingereza, ya kutaka kufuatilia watu waliohusika katika vita vya mauaji ya kimbari vinavyoendelea vya utawala wa Israel dhidi ya Gaza, ambavyo vilianza Oktoba 2023 na kusababisha zaidi ya Wapalestina 72,000 kuuawa shahidi.