Kiongozi wa harakati ya Kiislamu ya Ansarullah nchini Yemen amesema kuwa Marekani na Utawala wa Isael zinakabiliana na Iran kwa sababu Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inasimama kama kizuizi dhidi ya mradi wao mpana wa kutawala eneo la Asia Magharibi.

Akizungumza siku ya Ijumaa, Sayyid Abdul-Malik Badr al-Din al-Houthi alisema kuwa “adui wa Kizayuni, kwa kushirikiana na Marekani, analenga kuyatawala mataifa ya eneo hili,” akisisitiza kuwa sababu kuu ya kulengwa kwa Iran ni nafasi yake ya kuzuia na kudhoofisha njama hizo.

Aliitaja misimamo ya Iran kuwa “imara na thabiti,” akiielezea Tehran kama ngome imara inayokwamisha ajenda ya pamoja ya Marekani na Israel.

Kauli hizo zimekuja wakati kunashuhudiwa ongezeko la vitisho vya Marekani dhidi ya Iran, huku Rais wa Marekani Donald Trump akiendelea kutuma meli za kivita na vikosi vingine katika maeneo yaliyo karibu na Iran, sambamba na kuendelea kwa mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Washington na Tehran kuhusu suala la nyuklia.

Al‑Houthi amesema kuwa Umma wa Kiislamu kwa ujumla unakabiliwa na mashinikizo yanayoongezeka. “Umma unakumbwa na changamoto na kuna matatizo mengi katika ulimwengu wa Kiarabu na Kiislamu,” alisema, akionya kuwa changamoto hizo zinaibuka kwa wakati mmoja.

Ameongeza kuwa makabiliano hayo hayapo tu katika uwanja wa kijeshi au kisiasa. “Maadui, kupitia vita laini (soft war), wanajaribu kuukata uhusiano wa Umma na uongofu wa Mwenyezi Mungu na Uislamu, ili kusiwe na mshikamano wa kujikinga,” amesema.

“Leo tunakabiliwa na vita kubwa zaidi vya fikra tangu mwanzo wa jamii ya binadamu,” ameongeza, akielezea mapambano hayo kuwa ya kiitikadi pamoja na ya kijiografia na kisiasa.

Kiongozi huyo wa Yemen pia amekosoa hali ya kutojali inayosambaa katika mataifa ya Kiislamu. Amesema kuwa watu wengi wanapuuza hatari zinazoukabili Umma, lakini akaonya kuwa “uzembe huo hauna manufaa.” Amesisitiza kuwa kujitenga na wajibu na kubaki bila ufahamu wa uhalisia ni jambo “hatari.”

Ameendelea kusema kuwa Umma unakabiliwa na vitisho kutoka kwa “maadui wenye chuki yaani Uzayuni pamoja na matawi yake ya Kimarekani, Kizayuni cha Israel na Uingereza.”

Aidha amesema kuwa Israel inalenga kufuta urithi wa Kiislamu katika maeneo ya Palestina inayoyakalia  kwa mabavu kwa kubomoa maeneo ya kihistoria na kuwafukuza wakazi wake.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *