Meneja wa timu ya Manchester City, Pep Guardiola, amejibu maoni ya mmiliki wa Manchester United, Sir Jim Ratcliffe kuhusu uhamiaji, akisema kwamba kuna haja ya “kukumbatia tamaduni zingine ili kuifanya jamii iwe bora.”
Shirika la habari la Uingereza PA Media limeripoti kwamba Ratcliffe, mmiliki wa hisa za waliowachache wa Manchester United, alizua utata wiki hii baada ya kudai kwamba Uingereza “imekoloniwa na wahamiaji”.
Ratcliffe amelazimika kuomba msamaha baada ya matamshi yake kutajwa kuwa ni “ubaguzi wa rangi”.

Hata hivyo kocha wa Manchester City anaamini kuwa suala zima la jinsi nchi (za Magharibi) zinavyowashughulikia wahamiaji bado ni “tatizo kubwa”.
“Tatizo duniani kote ni kwamba tunawatamba wahamiaji au watu wanaotoka nchi nyingine kama chanzo cha matatizo ambayo nchi zetu zinapitia, na hili ni tatizo kubwa sana,” amesema Pep Guardiola na kuongeza: “Kila mtu anataka maisha bora na mustakabali bora kwa ajili yake mwenyewe, familia yake, na marafiki zake. Wakati mwingine fursa zinapatikana mahali ulipozaliwa, na wakati mwingine mahali unapoweza kwenda.”
Kocha huyo Mhispania ameeleza kuwa: “Watu wengi hukimbia nchi zao kwa sababu ya matatizo, si kwa sababu wanataka kuondoka. Kadiri tunavyokumbatia tamaduni nyingine – kwa dhati na kwa undani – ndivyo tutakavyokuwa jamii bora.”
Amesema: “Mimi kuwa Mkatalani hakunifanyi nijisikie bora zaidi kuliko wewe.”