
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imelaani vikali uamuzi wa hivi karibuni wa utawala ghasibu wa Israel wa kunyakua ardhi zaidi za Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu, ikisema hatua hiyo inalenga kupanua ‘ujenzi wa vitongoji haramu’ na kuimarish uvamizi na udhibiti wa masuala ya usalama katika eneo hilo, sambamba na kuendeleza ‘mauaji ya kimbari’ ya Gaza.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmaeil Baqaei, ameashiria mauaji yanayoendelea kufanywa na Israel dhidi ya watu Palestina huko Gaza na Ukingo wa Magharibi na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu na sheria za kibinadamu, ikiwa ni pamoja na kuendelea kuwashikilia Wapalestina kinyume cha sheria magerezani na mateso makali ya wafungwa wa Kipalestina.
Amevitaja vitendo hivyo kuwa mienendo ya kijinai inayofanywa sambamba na sera ya mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina na kutokomeza Palestina kikoloni, na kusisitiza “wajibu wa pamoja wa nchi zote kuzuia mauaji ya kimbari ya watu wa Palestina na unyakuzi wa ardhi zao.”
“Kutokujali kwa utawala wa Israel na uungaji mkono mkubwa wa Marekani na baadhi ya nchi za Ulaya, hasa Ujerumani na Uingereza, ni miongoni mwa sababu za kuendelezwa mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina,” amesema Esmaeil Baqaei.
Pia ameukosoa vikali Umoja wa Mataifa na vyombo vingine vya kimataifa kwa kutochukua hatua yoyote ya maana ya kukabiliana na sera za kikoloni na za kujipanua za utawala wa Israel.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ametili mkazo msimamo wa kimsingi wa Jamhuri ya Kiislamu katika kuunga mkono mapambano ya “kurejeshwa haki halali za watu wa Palestina, hasa haki ya kujitawala, kujikomboa kutoka kwenye uvamizi na kuanzisha taifa huru la Palestina, mji mkuu wake ukiwa Al-Quds al-Sharif.
Utawala wa Israel umeidhinisha mfululizo wa hatua kali katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu ambazo Wapalestina wanaonya kuwa ni uvunjaji wa wazi wa Makubaliano ya Oslo na unyakuzi mwingine wa ardhi ya Palestina.