Madagascar, kisiwa kikubwa zaidi barani Afrika na makao ya jamii ya Malagasy, iliingia katika moja ya vipindi vya giza zaidi katika historia yake mwishoni mwa karne ya 19.

Ufaransa, mojawapo ya mataifa muhimu zaidi ya kikoloni ya wakati huo, iliitangaza Madagascar kuwa koloni lake mwaka wa 1896, kwa lengo la kupanua ushawishi wake wa kisiasa na kiuchumi na kudhibiti maliasili za kisiwa hicho. Kabla ya hapo, Ufaransa ilikuwa na miongo kadhaa ya uingiliaji mdogo wa kisiasa na kijeshi katika kisiwa hicho, na hivyo kuandaa mazingira ya utawala na satua kamili.

Lengo la Ufaransa lilikuwa kuunda serikali kuu yenye kudhibitika ambayo ingewalazimisha watu wa asili kufanya kazi za kulazimishwa na kutoa maliasili za kisiwa hicho. Ili kufikia malengo haya, Ufaransa ilibadilisha haraka miundo ya kisiasa, kiuchumi, na hata kijamii ya Madagascar. Sheria mpya zilizuia umiliki wa ardhi wa watu wa asili, kazi za kulazimishwa na kodi kubwa ziliwekwa kwa watu, na udhibiti wa moja kwa moja wa maliasili na mashamba makubwa ulipangwa na Wafaransa. Hata lugha na mfumo wa elimu wa Kifaransa ulibadilisha mila na elimu ya wenyeji. Kwa hatua hizi, kivitendo Ufaransa iliharibu utawala wa kitamaduni wa kifalme na nguvu ya wazee wa eneo hilo. Hatua hizi hazikutishia tu maisha ya kila siku na uhuru wa watu wa Madagascar, lakini pia zilifanya hali kuwa ngumu na isiyovumilika kwao, na watu wakawa wafanyakazi wa Ufaransa ambao walilazimika kufanya kazi katika sekta mbalimbali kulingana na maagizo ya waajiri wa Ufaransa. Hali hii ilifungua njia ya kuundwa upinzani wa watu wengi nchini Madagaska na kuibua hasira na malalamiko makubwa miongoni mwa watu wa kiasili kote nchini humo.

Tangu mwanzo kabisa wa uvamizi wa Wafaransa nchini Madagascar, upinzani wa umma ulianza. Mojawapo ya harakati za kwanza ilikuwa Uasi wa Menalamba. Watu wa asili walianzisha harakati wakitoa radiamali yao kwa kuanguka utawala wa kifalme na mashinikizo la Ufaransa. Mwanzoni harakati hizi zilikuwa za wenyeji, lakini zikiwakilisha upinzani mkubwa wa umma kwa sera za kikoloni za Ufaransa. Radiamali ya Wafaransa kwa harakati hizi ilikuwa ya kikatili. Vikosi vya kikoloni vikijaribu kuimarisha udhibiti wa kisiwa hicho, vilifanya mauaji ya halaiki, mateso, na kuuwapeleka uhamishoni viongozi wake na kudhihirisha wazi  utumiaji mabavu wa kimfumo.

Mwaka 1947 Ufaransa ilifanya mauaji makubwa nchini Madagascar

Mojawapo ya upinzani mkubwa na wa umwagaji damu zaidi ulianza Machi 29, 1947, harakati kubwa ya watu wajamii nya Malagasy dhidi ya utawala wa kikoloni wa Ufaransa. Uasi huo, ulioanza katika majimbo ya Moramanga na Manakara, na Vohipeno, ulienea katika sehemu kubwa za kisiwa hicho ndani ya miezi michache. Watu waliingia mitaani, hasa wakiwa na silaha za awali kabisa, na kwa nia ya uhuru na kukomesha utawala wa kigeni. Makadirio yanaonyesha kwamba zaidi ya watu milioni moja walishiriki katika uasi huo, wakionyesha kina cha hasira na hamu ya uhuru katika jamii yote ya Malagasy.

Jibu la Wafaransa kwa uasi huo lilikuwa mojawapo ya ukandamizaji wa kikatili zaidi katika historia ya ukoloni. Kamandi ya kikosi cha kikoloni nchini Madagascar, ikiongeza idadi ya wanajeshi hadi takriban 18,000 na kuhamisha wanajeshi kutoka sehemu zingine za himaya yake, ilitekeleza sera ya ugaidi na ukandamizaji ulioenea, na ilitumia wanajeshi mahiri, wanajeshi wa parachuti, na wanajeshi kutoka makoloni mengine kukandamiza uasi huo.

Mbali na mauaji ya halaiki na mateso, jeshi la Ufaransa lilichoma vijiji vingi na kuwaua wakazi wake kwa umati. Ubakaji wa kijeshi na unyanyasaji wa kingono dhidi ya wakazi ulikuwa umeenea, na hakukuwa na kikomo cha ukandamizaji wa raia. Vitendo hivi vya kikatili vinatoa picha ya wazi ya ukubwa wa ukandamizaji wa Ufaransa nchini Madagascar.

Mojawapo ya mbinu za ukandamizaji, ambazo hazijawahi kutokea katika historia ya ukoloni, ambazo baadaye zilijulikana kama “ndege za kifo”, zilikuwa za kutisha na zisizo za kibinadamu kiasi kwamba bado zimeandikwa katika kumbukumbu ya kihistoria ya Madagascar na ulimwengu. Katika mbinu hii, wafungwa hai, ambao mara nyingi walikuwa wamefungwa pingu, walitupwa kutoka kwenye ndege ili wafe. Njia hii haikutumika tu kuua watu mara moja, bali pia kusababisha hofu kubwa na msambaratiko wa kisaikolojia miongoni mwa watu. Lengo la Wafaransa la hatua hii lilikuwa kuonyesha nguvu yao kamili na kukandamiza upinzani wowote unaowezekana; ili watu wasithubutu tena hata kufikia maeneo ya mkusanyiko wa vikosi vya Ufaransa.

Jamii ya Malagasy

Ukweli wa mambo ni kuwa, safari za kifo hazikuwa tu operesheni ya kijeshi; zilikuwa zana ya kisaikolojia na ugaidi mkubwa uliokusudiwa kuwatisha watu wote na kusambaratisha azma na irada yao. Wafungwa kwa kawaida walishikiliwa katika hali zisizo za kibinadamu na kuteswa awali, na kisha kutupwa kutoka juu bila uwezekano wowote wa kujilinda. Safari za kifo zilikuwa nembo ya ukatili mkubwa wa vikosi vya kikoloni vya Ufaransa; mfano ambao haukuwa ukiharibu tu miili ya watu, lakini pia uliziacha roho na nafsi za watu katika hali ya mshtuko na hofu kwa miongo kadhaa.

Kwa akali ukatili huu uliua watu 30,000 hadi 40,000, na baadhi ya makadirio yanataja idadi hiyo kuwa zaidi ya 100,000. Sehemu kubwa ya waathiriwa walikuwa raia, wengi wao wakiwa wanawake, watoto na wazee.

Hii leo, Machi 29 inaadhimishwa kila mwaka kama siku ya kukumbuka wahanga wa ukatili huu nchini Madagascar. Siku hii sio tu inawakumbuka wahanga, lakini pia inaikumbusha jamii kwamba, utawala wa kikatili na unyonyaji hauwezi kufutwa kutoka katika kumbukumbu ya pamoja, hata baada ya miongo kadhaa. Safari za kifo, mateso ya kimfumo na mauaji ya halaiki ni mifano ya ukubwa wa ukatili wa kikoloni wa Ufaransa dhidi ya watu; uhalifu unaoonyesha kwamba, ili kudumisha madaraka hakuna mipaka katika kutenda ukatili.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *