Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anayehusika na masuala ya kisiasa amesema ni zamu ya Marekani kuonyesha azma ya kufikia makubaliano yanayolenga kutatua suala la nyuklia la Tehran.

Majid Takht-Ravanchi ametoa matamshi hayo katika mahojiano na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) yaliyochapishwa leo Jumapili, zaidi ya wiki moja baada ya maafisa wa Iran na Marekani kufanya mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja nchini Oman kufuatia wiki kadhaa za mvutano unaoongezeka unaosababishwa na vitisho vya vita ya Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.

Amesema, mpira uko “kwenye uwanja wa Marekani kuthibitisha kwamba inataka kufanya makubaliano,” akiongeza kuwa: “Ikiwa ni wakweli, nina uhakika tutakuwa njiani kuelekea kwenye makubaliano.”

Takht-Ravanchi, mjumbe wa timu ya mazungumzo ya Iran, pia amesema kwamba Washington imeonyesha nia ya kutatua masuala yaliyopo kwa amani, hadharani na faraghani, kupitia Oman.

Wakati huo huo, mwanadiplomasia huyo wa Iran ameonya kwamba vita vingine vitakuwa “vya kutisha, vibaya kwa kila mtu … kila upande utaumia, haswa wale watakaoanzisha uchokozi huo.”

Takht-Ravanchi amesema kwamba mazungumzo ya hivi karibuni kati ya Iran na Marekani katika mji mkuu wa Oman, Muscat yamekuwa “kwa kiasi fulani katika mwelekeo mzuri, lakini ni mapema mno kuhukumu.”

Pia amethibitisha kwamba duru ya pili ya mazungumzo hayo inatarajiwa kufanyika katika jiji la Geneva nchini Uswisi siku ya Jumanne.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *