Mwanajeshi mmoja katika jeshi la Israel ametoa kauli ya kushtua katika mahojiaano ya moja kwa moja na YouTuber wa Marekani, akizungumzia vitendo vinavyofanywa na wanajeshi wa utawala huo dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza katika vita vya mauaji ya kimbari.

Hatuui tu, lakini pia tunabaka,” ni maneno yaliyosemwa na mwanajeshi huyo wa Israel wakati wa matangazo ya moja kwa moja kwenye TikTok na YouTuber wa Marekani anayeitwa Jeff Davidson, akieleza uhalifu unaofanywa na Israel dhidi ya watu wa Gaza. Mwanajeshi huyo amesema kwamba kwa sasa anahudumu katika jeshi la Israel huko Gaza, akionyesha picha ya uharibifu uliofanywa katika eneo lake na akasema: “Usishangae, hakuna nyumba hapa, zimebomolewa kabisa,” alipoulizwa: “Ninyi ndio mmeziharibu,” amejibu kwa kusema: “Ndiyo.”

Mwanajeshi huyo wa Israel amesema: “Tumewaua wanawake na watoto,” akiongeza: “lakini pia, tunawabaka”.

Video hiyo imeibua hasira kubwa kwenye mitandao ya kijamii, huku wanaharakati wakiitaja kauli ya mwanajeshi huyo wa Israel kuwa ni “ushahidi mzito” wa uhalifu ambao jeshi la Israel linashutumiwa kufanya dhidi ya raia katika Ukanda wa Gaza.

Watumiaji wa mitandao ya kijamii wanasema kwamba kauli kama hizo zinaonyesha hisia ya kukingiwa kifua na kukwepa adhabu, wakisema kwamba himaya ya kisiasa ambayo serikali ya Israel, inayoongozwa na Benjamin Netanyahu, inapewa na Marekani na nchi kadhaa za Magharibi inachangia katika ukosefu wa uwajibikaji wa kimataifa.

Ikumbukwe kuwa, Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limethibitisha katika ripoti yake ya kila mwaka iliyotolewa leo Jumatano kwamba katika mwaka mzima wa 2025 Israel ilifanya uhalifu wa kivita, uhalifu dhidi ya ubinadamu, vitendo vya mauaji ya kimbari na maangamizii ya kizazi dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi, na kusababisha vifo, majeraha na kuhamishwa kwa lazima mamia ya maelfu ya watu, kwa kushirikiana na Marekani.

Katika ripoti ya hali ya haki za binadamu katika zaidi ya nchi 100 mwaka jana, shirika hilo limesisitiza kwamba uhalifu wa Israel mwaka 2025 ulifanyika kwa kiwango “ambacho hakijawahi kutokea katika historia ya hivi karibuni ya Israel na Palestina.”

Gaza

Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch lenye makao yake makuu huko New York City nchini Marekani limesema kwamba idadi ya Wapalestina waliouawa mwaka jana kutokana na uhalifu wa Israel ni kubwa kuliko makadirio ya Wizara ya Afya ya Gaza, hasa kwa vile takwimu zake za waliouawa hazijumuishi wale waliozikwa chini ya vifusi au wale waliokufa kutokana na magonjwa, njaa na kiu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *