Ukraine. Beki wa zamani wa Manchester City na Arsenal, Oleksandr Zinchenko (29) kwa sasa ni baba wa watoto wawili katika ndoa na mpenzi wake wa kitambo, Vlada Sedan (30), ambaye ni wanahabari kutokea huko kwao Ukraine.
Ndoa na familia kwa ujumla vimekuwa sehemu ya kazi zao za kila siku, mathalani mapema mwezi huu, wakati Zinchenko akiwaaga Arsenal na kujiunga na Ajax, Vlada aliungana naye kutoa neno la shukrani.
“Ni wakati wa kufungua ukurasa mwingine katika hadithi yetu ya soka. Daima Arsenal itabaki ikihusishwa na kumbukumbu nyingi za furaha, ukarimu na upendo,” anaeleza Vlada.
“Ilikuwa heshima kubwa sana kwetu kuwa sehemu ya klabu kubwa kama hii. Asanteni kwa kila kitu. Kila la kheri, Gunners,” aliandika Vlada katika ukurasa wake wa Instagram mnamo Februari, Mosi.
Zinchenko alithibitisha uhusiano wake na Sedan pindi alipoonekana akimpiga busu mrembo huyo baada ya timu yao ya taifa ya Ukraine kuibuka na ushindi mnono wa mabao 5-0 dhidi ya Serbia mnamo Juni 2019.
Hii ilikuwa ishara kwamba beki huyo hakuwa tu anampenda Sedan, bali alikuwa tayari kumuweka mbele katika maisha yake kwa muda wote na ndivyo ilivyo hadi wakati huu.
Kabla ya tukio hilo, kwa miezi kadhaa nyuma mashabiki walikuwa wakijiuliza ikiwa ni kweli wawili hao ni wapenzi lakini wachezaji wenzake ndani ya Man City, tayari walikuwa wanafahamu kinachoendelea.
Wawili hao walifunga ndoa Agosti 2020, mwaka mmoja baada ya Zinchenko kumvisha Sedan pete ya uchumba ndani ya uwanja wa Olimpiki wa Kiev wenye uwezo wa kubeba watu takribani 70,000.
Kutoka kipindi cha uchumba hadi kuwa na familia yenye watoto wawili, wawili hawa wameendelea kuwapa mashabiki picha halisi ya penzi linaloishi ndani na nje ya uwanja.
Mtoto wao wa kwanza, Eva, alizaliwa Agosti 1, 2021 ikiwa ni mwaka mmoja baada ya ndoa, huku wa pili, Leia akizaliwa hapo Agosti 2, 2023, hii ina maana kuwa watoto hao husherehekea birthday zao kwa kufuatana.
Mtoto huyo wa pili alizaliwa siku chache kabla ya mechi ya hisani iliyoandaliwa na Zinchenko kusaidia taasisi yake pamoja na tovuti ya kuchangisha fedha ya United24, iliyoanzishwa baada ya Urusi kuivamia Ukraine.
Picha zao kama familia ambazo wamekuwa wakiziposti mtandaoni zimekuwa zikionyesha tabasamu, upendo na umoja. Kwa mashabiki, huu ni uthibitisho kuwa mafanikio ya kweli si tu yale ya kazini, bali pia yale ya nyumbani.
Machi 2025, Vlada alikuwa anasherehekea kutimiza umri wa miaka 30, tofauti na miaka mingine hii ilikuja tofauti baada ya kupokea ujumbe wa kushtukiza kutoka kwa David Beckham.
Wakati huu Zinchenko alikuwa akiichezea Nottingham Forest kwa mkopo, na ndipo akiwa na marafiki zake akampigia (video call) Vlada kisha akampa Beckham nafasi ya kuzungumza naye.
“Habari Vlada, unaongea hapa na David Beckham. Nilitaka tu kukutumia ujumbe kwa sababu nimesikia ni siku yako ya kuzaliwa,” alisema Beckham na kuongeza.
“Nina uhakika utakuwa na siku ya kipekee pamoja na mume wako na familia. Nakutakia furaha na heri ya kutimiza miaka 30,” anasema gwiji huyo wa England, Manchester United na Real Madrid.
Vlada kupitia ukurasa wake wa Instagram wenye wafuasi zaidi ya 657,000, alisema kuwa ujumbe huo wa Beckham ulimtoa machozi kutokana na heshima aliyonayo katika ulimwengu wa soka.
Mbali na uhusiano wake na Zinchenko, Vlada ni mwandishi wa habari za michezo mwenye jina kubwa aliyewahi kuwahoji mastaa wakubwa wa soka kama Cristiano Ronaldo.
Umahiri wake mbele ya kamera, ujasiri na urembo wake vilimfanya awe maarufu hata kabla ya ndoa. Lakini pamoja na hadhi hiyo, aliweka wazi kuwa moyo wake uko kwa mwanaume mmoja tu, naye ni Zinchenko.
Akiwa katika kazi anasimamia kila anachokiamini, mathalani kuna wakati ambapo alimkosoa Pep Guardiola hadharani kutokana na mbinu zake za ulinzi, hatua iliyomlazimu Zinchenko kuomba radhi kwa niaba yake.
Zinchenko ambaye bado alikuwa akiitumikia Man City, anasema kuwa mke wake aliongea kama shabiki akieleza hisia zake kwa lengo la kutaka timu ifanye vizuri na si vinginevyo.
“Ingawa mke wangu ni mwandishi wa habari, pia ni shabiki. Msimu mzima alikuwa akisafiri nasi kwenye mechi za ugenini na nyumbani kwa sababu ni shabiki mkubwa wa Man City.
“Tunaelewa hakupaswa kuiweka video hiyo mitandaoni kwa sababu yeye ni mke wangu. Lakini hakutoa maoni kama mwandishi kuhusu kocha, bali alikuwa anaonyesha tu maumivu yake kama shabiki,” anaeleza.
Kwa sasa anaonekana kujikita katika malezi ya familia na kuipa kisogo kazi yake, ni mfano wa mama bora kwa watoto wake. Naye Zinchenko, licha ya ratiba ngumu za soka, hujitahidi kutumia muda mwingi na familia yake.