
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araqchi, amewasili katika miji wa Geneva nchini Uswisi kwa ajili ya duru ya pili ya mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja na Marekani kuhusu mpango wa nyuklia wa amani wa Jamhuri ya Kiislamu.
Araqchi, ambaye alitua Geneva usiku wa kuamkia leo, anaandamana na ujumbe wa kidiplomasia na wataalamu wa ngazi ya juu.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran alikuwa ametangaza hapo awali kwamba Araqchi pia anatarajiwa kufanya mikutano ya kidiplomasia kando ya mazungumzo hayo.
Duru ya pili ya mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Iran na Marekani itafanyika Jumanne wiki hii kwa upatanishi wa Oman.
Duru ya kwanza ya mazungumzo hayo ilifanyika katika mji mkuu wa Oman, Muscat mapema mwezi huu.
Huko Geneva, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran atakutana na mwenzake wa Uswisi, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki na viongozi wengine mashuhuri wa kimataifa.
Akizungumza mwishoni mwa mazungumzo yaliyosimamiwa na Oman, Sayyid Abbas Araqchi alisema mazungumzo na Marekani yalikuwa “mwanzo mzuri” na yanaweza kuendelea.
Matakwai makuu ya Iran huko Muscat yanabaki kuwa kuondolewa vikwazo vya kiuchumi.