
Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan ametuma salamu za rambirambi kwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, kufuatia kifo cha mwanamuziki mkongwe, Steven Hiza kilichotokea jana jioni nyumbani kwake jijini Tanga.
Samia ametoa pole hizo kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii pamoja na taarifa iliyotolewa na Shaaban Kissu, mkurugenzi msaidizi Mawasiliano ya Rais, Ikulu, akiahidi kuenzi mchango wake katika sekta ya muziki hasa kupitia wimbo wa ‘Tanzania Yetu’.
“Rais Dk Samia amemtaja Marehemu Hiza kuwa msanii mahiri na mzalendo aliyetumia kipaji chake kuelimisha, kuburudisha na kuhamasisha jamii, huku akitumia sanaa kama chombo cha kuimarisha maadili, umoja na utambulisho wa Taifa.
“Marehemu, aliyewahi kuhudumu katika bendi ya muziki ya Atomic Jazz Band, atakumbukwa kwa mchango wake mkubwa katika kukuza na kuendeleza muziki wa Tanzania, hususan kupitia wimbo wake maarufu wa “Tanzania Yetu ndiyo Nchi ya Furaha,” wenye hisia za uzalendo na mshikamano wa kitaifa,” ameandika
Rais pia ameendelea kutoa rai kwa wasanii akiwataka kudumisha uzalendo katika kazi za sanaa.
“Vilevile, Rais Dk Samia ametoa rai kwa wanamuziki na wadau wa tasnia ya muziki nchini kudumisha na kuenzi mchango wake kwa kuendeleza misingi ya uzalendo, ubunifu na uzalishaji wa kazi za sanaa zenye tija kwa Taifa.
“Rais Samia anatoa pole kwa familia ya Marehemu, ndugu, jamaa, wanamuziki, wadau wa sanaa na Watanzania wote kwa ujumla. Aidha, anawaombea wafiwa uvumilivu, faraja na moyo wa subira katika kipindi hiki kigumu cha msiba, huku akimuomba Mwenyezi Mungu ailaze roho ya Marehemu Steven Hiza mahali pema peponi, amina”
Enzi za uhai wake Mzee Hiza alijulikana kupitia wimbo wa ‘Tanzania Yetu’ ambao umekuwa maarufu na wenye kukonga nyoyo ukielezea uzalendo, mshikamano na umoja wa Watanzania. Wimbo huo aliutunga akiwa na Bendi ya Atomic Jazz ya Tanga kati ya mwaka 1966 na 1967.