Dar es Salaam. Nguli wa Bongo Fleva, Joseph Haule (Profesa Jay) amefunguka kurudi upya jukwaani, akisisitiza anarudi kupindua meza kwenye tasnia ya muziki.

Jay atapanda jukwaani Ijumaa ya Mei Mosi kufanya shoo kwenye Bongo Fleva Honors inayoandaliwa na Deiwaka World.

Nguli wa Bongo Fleva, Joseph Haule maarufu Profesa Jay (wa kwanza kushoto) akipeana mkono na muasisi wa Bongo Fleva Honors, Joseph Mbilinyi maarufu Sugu leo Jumanne Februari 17, 2026 baada ya kusaini makubaliano ya kufanya shoo Mei Mosi

Akizungumza leo Februari 17, 2026 wakati wa kutambulisha msimu wa nne wa Bongo Fleva Honors unaofunguliwa na yeye Jay, amesema anarejea rasmi kwenye gemu baada ya kuwa nje kwa muda mrefu kutokana na masuala mbalimbali ikiwamo ya kiafya.

Amesema anajipanga kufanya shoo kubwa kuliko zote alizowahi kuzifanya, shoo ambayo ndiyo inakwenda kumrudisha rasmi kwenye gemu ya muziki wa Bongo Fleva. 

“Yule profesa Jay wa mitulinga sasa yupo fiti nitaanzia mwanzo nilipoanzia Bongo Fleva hadi nilipoishia, wasanii ambao nimefanya nao kazi watakuwepo wengi ku show love (kumuunga mkono), siku hiyo itakuwa ni zaidi ya shoo,” amesema Jay.

Akizungumzia maandalizi ya shoo hiyo, muasisi wa Bongo Fleva Honors, Joseph Mbilinyi (Sugu) amesema anayekwenda kuwafungulia msimu mpya ni mkongwe asiye na shaka akimtaja kuwa ni heavy weight.

“Muda umefika sasa kumheshimisha Profesa Jay wa mitulinga,” amesema Sugu.

Nguli wa Bongo Fleva, Joseph Haule maarufu Profesa Jay (wa kwanza kushoto) akizungumza na waandishi wa habari leo Jumanne Februari 17, 2026 kuhusu shoo yake ya Bongo Fleva Honors itakayofanyika Mei Mosi.

Amesema kikawaida msimu mpya wa Bongo Fleva Honors huanza mwanzoni mwa mwaka, lakini kutokana na mazingira walilazimika kusogeza mbele.

“Sasa ni wakati sahihi kuwapelekea mashabiki burudani,” amesema Sugu akibainisha kwamba shoo hiyo itafanyika jijini Dar es Salaam na taratibu zingine zitatangazwa wiki tatu kabla ya siku ya shoo ya Mei Mosi.

Amesema katika msimu wa nne anayekwenda kuwafungulia ni mkongwe asiyena shaka heavy weight, Profesa Jay ambaye hakuna asiyejua mchango wake kwenye muziki wa Bongo fleva.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *