
Unguja. Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kupitia Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale pamoja na Wizara ya Kazi na Uwekezaji, zimesaini makubaliano ya ushirikiano na kampuni ya Infinity Developments kurejesha na kuhuisha maeneo muhimu ya kihistoria na urithi wa Zanzibar.
Katika mpango huo, kampuni hiyo inatarajia kutumia Dola za Marekani 12 milioni (Sh30.907 bilioni) awamu ya kwanza katika maeneo muhimu yaliyopo ndani ya tovuti ya Urithi wa Dunia ya (Unesco) ya Mji Mkongwe (Stone Town), ambayo ni bustani ya Tenga, Afrika House na jengo la kihistoria la wakf la Khoja Ismailia.
Akizungumza leo Februari 19, 2026 katika hafla hiyo, Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dk Aboud Suleiman Jumbe amesema makubaliano hayo yanaashiria mwanzo mpya wa maendeleo ya kiutamaduni na kiuchumi Zanzibar, yakiiweka hifadhi ya urithi kuwa nguzo kuu ya kukuza utalii endelevu.
Amesema hatua hiyo, pia, imesaidia kupunguza mzigo mkubwa wa bajeti ambao Serikali imekuwa ikiubeba kila mwaka katika kusimamia uhifadhi, ukarabati na uendelezaji wa maeneo ya kihistoria Unguja na Pemba.
Amesema kupitia mpango wake wa Infinity Culture Programu, Infinity Developments imejitolea kuwekeza takribani Dola za Marekani milioni 12 kwa awamu ya kwanza ya marejesho, uboreshaji wa miundombinu, kazi za uhifadhi na kuboresha uzoefu wa wageni.
Naye Mkurugenzi Mtendaji na Mwenyekiti wa Infinity Developments, Samuel Saba amesema moja ya mambo yanayoitofautisha Zanzibar na visiwa vingine duniani, mbali na watu wake wenye ukarimu wa kipekee, ni utamaduni na historia yake.
Amesema utamaduni na historia ya Zanzibar ndivyo vinavyoipa upekee mkubwa unaoiwezesha kushindana na visiwa vingine vyote, si barani Afrika pekee bali duniani kote.
“Sio tu kwa kiwango cha jamii au kampuni katika sekta nzima, bali pia tuna dhamira ya kuwekeza katika sekta hii ya utalii wa urithi wa kitamaduni, tunaamini kutokana na ukuaji mkubwa ambao tumeuona visiwani kufuatia sera madhubuti zilizowekwa na Serikali,” amesema.
“Tunashukuru na tunajivunia heshima tuliyopewa, kwani kukamilika kwa miradi hii, tunaamini kwa kiasi kikubwa itachangia kuongeza kuridhika, kuimarisha fahari ya kitamaduni, na kuendeleza juhudi za ukarabati,” amesema.