
Dar es Salaam. Ni mwendo wa zimamoto. Hatimaye dirisha la uchukuaji na urejeshaji fomu limefunguliwa kwa makada wa Chama cha Wananchi (CUF) wanaotaka kuingia kwenye kinyanganyiro cha kuwania nafasi tatu za juu ndani ya chama hicho, ikiwemo nafasi ya mwenyekiti wa Taifa.
Nafasi nyingine zitakazoshindaniwa ni Makamu Mwenyekiti Tanzania Bara na Makamu Mwenyekiti Zanzibar.
Hatua hiyo imefikiwa kufuatia maazimio ya kikao cha Baraza Kuu la chama hicho lililoketi leo, ambapo limesisitiza kuwa mwisho wa kurejesha fomu ni kesho saa 2 asubuhi.
Kwa mujibu wa Baraza hilo, ambalo wakati fulani liligubikwa na vurugu, kelele na baadhi ya wajumbe kujikuta mikononi mwa polisi na kutolewa nje ya ukumbi baada ya fomu kurejeshwa, kutafanyika kikao cha dharura cha kufanya mchujo wa majina.
Watakaokidhi vigezo kwa mujibu wa Katiba na taratibu za chama, watakwenda kupigiwa kura na wajumbe wa mkutano mkuu wa dharura unaotarajiwa kufanyika kesho katika Ukumbi wa Lekham, mkabala na ofisi za makao makuu ya chama hicho, Buguruni.
Hatua hizo zinachukuliwa wakati chama hicho kinakabiliwa na mgogoro wa uongozi uliowagawa wanachama katika pande mbili, kufuatia uamuzi wa Msajili wa Vyama vya Siasa kufuta uchaguzi uliofanyika Desemba 18 na 19, 2024, uliomweka madarakani Profesa Ibrahim Lipumba na wenzake watano.
Sababu ya kufutwa kwa uchaguzi huo ni kwamba Profesa Lipumba na wenzake hawakupata zaidi ya nusu ya kura halali zilizopigwa na wajumbe. Kwa kuzingatia Katiba na taratibu za chama, mchakato huo ulipaswa kurudiwa ili kukidhi matakwa ya kisheria.
Uamuzi huo umeibua mgawanyiko miongoni mwa wanachama. Kundi moja linajiandaa kwenda mahakamani kupinga uamuzi wa Msajili uliotolewa Februari 13, 2026, wakidai haukuzingatia haki za msingi, ikiwemo haki ya kusikilizwa.
Hata hivyo, kundi jingine linaunga mkono uamuzi huo, likiwemo lile lililokuwa likilalamikia mchakato wa awali kuwa haukuzingatia haki. Kundi hilo sasa limeanza kutekeleza maelekezo ya Msajili kwa kuanza mchakato wa kupata uongozi mpya.
Akizungumza leo Februari 2026 baada ya kikao hicho, katibu wa kikao ambaye pia ni mwenyekiti wa chama Wilaya ya Tanga, Mussa Mbarouk amesema mkutano umefanyika kwa amani licha ya kuwapo kwa mvutano wa hapa na pale.
“Baraza Kuu kwa kauli moja limeazimia yafuatayo: Kwanza, mkutano mkuu wa dharura utafanyika kesho Jumamosi kwa ajili ya uchaguzi wa viongozi wapya. Kwa msingi huo, dirisha la uchukuaji na urejeshaji fomu limefunguliwa kuanzia saa 8 mchana na litafungwa kesho saa 2 asubuhi,” amesema.
Amesema wanachama wote wenye sifa za kuhudumu ndani ya chama kwa angalau miaka miwili, wanaruhusiwa kuchukua fomu katika makao makuu ya chama ili kushiriki katika mchakato huo.
“Baada ya kufungwa kwa dirisha la uchukuaji na urejeshaji fomu, kutafanyika kikao kidogo cha dharura kwa ajili ya kufanya mchujo. Wataokidhi vigezo kwa mujibu wa Katiba na taratibu zetu watawasilishwa kwenye mkutano mkuu wa dharura ili wajumbe wawapigie kura,” amesema Mbarouk.
Ameongeza uamuzi wa kikao hicho ni halali kwa kuwa wajumbe 27 kati ya 43 waliopo walishiriki, hivyo hakuna sababu ya kuendelea kusuasua badala yake wajumbe wanapaswa kujiandaa kupata uongozi mpya na kuhitimisha kipindi cha mpito.
“Mkutano Mkuu unatarajiwa kufanyika katika Ukumbi wa Lekham hapa Buguruni kuanzia saa 4 kamili asubuhi. Huu ni wakati wa wajumbe kutumia fursa hii kuchagua viongozi watakaotuongoza kwa kipindi cha miaka mitano,” amesema.
Kwa upande wake, Mohammed Nassor, mjumbe wa Mkutano Mkuu aliyesafiri kutoka Pemba, amesema lengo lake ni kutumia haki yake ya kupiga kura kuchagua viongozi anaowaona wanafaa.
“Si vyema chama kukaa bila uongozi; mali zinaweza kupotea na shughuli zikadorora. Licha ya tofauti zilizopo, nawaomba wenzetu wenye msimamo tofauti tuungane kwa pamoja,” amesema Nassor.
Msimamo wa upande wa pili
Akizungumzia suala hilo, Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Bara, Magdalena Sakaya amesema hajapokea taarifa rasmi ya kikao hicho, ingawa amesikia kuwa baadhi ya wajumbe walikamatwa na Polisi.
“Hatujapewa taarifa za kikao hicho. Msimamo wetu haujabadilika; tutaenda mahakamani kutafuta haki dhidi ya uamuzi wa Msajili kwa kuwa tunaamini hatukutendewa haki,” amesema.
Alipoulizwa ni lini watafungua kesi hiyo, Sakaya amejibu walikuwa wamepanga leo, lakini kwa taarifa ambazo Mwananchi imezipata, hakuna kesi ilifunguliwa.
Ikiwa wataendelea na msimamo huo, tafsiri yake ni kwamba mwenyekiti wa muda mrefu wa chama hicho, Profesa Lipumba hatakuwa miongoni mwa wanaotarajiwa kuingia katika kinyanganyiro hicho.