Dar es Salaam. Mwaka 1999 akiwa bado binti, alipendelea sana kutazama namna filamu zinavyoandaliwa. Ingawa  ndoto yake haikuwa katika ulimwengu huo,  lakini jicho la mwalimu wa kundi la ‘Afreeat’ liliona kitu cha tofauti ndani yake.

Ni Hidaya Njaidi ambaye kwa sasa anafanya vizuri katika tasnia ya filamu nchini. Akiwa ameonekana katika filamu mbalimbali ikiwemo Simcard, Family, Heshima ya Ndoa Situationship na nyinginezo.

Akizungumza na Mwananchi, Hidaya amefichua siri inayomfanya aendelee,  kuupiga mwingi katika tasnia ya filamu, akitaja nidhamu ya kazi kuwa msingi wa mafaniio yake.

“Kinachofanya nidumu hadi kuwa nguli katika tasnia hii ni nidhamu ya kazi. Na kuheshimiana na wasanii wenzangu pamoja na jamii kwa ujumla, kupitia mafunzo ninayoyapata kutoka kwa waongozaji wa filamu na malezi niliyolelewa tangu nilipoanza.

“Nilianza mwaka 1999 kuingia kwenye sanaa, baada ya mdada aliyekuwa mwigizaji kushindwa kufanya kilichotakiwa wakati wa mazoezi. Mimi nilienda kama mtazamaji, lakini mwalimu wa kundi la Afreeat, marehemu Chaiba Kombo, pamoja na mwalimu Kimela Biila wakaniambia: “Hidaya, utaweza kufanya tunacho muonesha huyu?” Nikasema ndiyo. Nikaingia mzogoni kujaribu, nikafanikiwa na huo ndio ukawa mwanzo wangu hadi leo nilipofikia hapa,”amesema Hidaya

Kama ilivyo kawaida  kila kazi huwa na changamoto zake. Hadija anaelezea mambo asiyopenda.

“Changamoto ambazo nakutana nazo mara nyingi hutokea kwa waandaaji wachanga. Kwa kuwa nataka nao waendelee kupiga hatua, huwa nashiriki baadhi ya kazi zao. Lakini wakati mwingine, wao hawajui kupangilia vizuri mambo yao, na kusababisha vitu haviendi sawa. 

“Sio kwa makusudi, bali ni kwa uchanga wao. Mimi ni mtu mwenye shughuli na majukumu mengi, hivyo nataka tukipanga muda tuutumie vizuri. Hii ni muhimu kwani mtu anaponipata, ina maana kwamba kuna baadhi ya shughuli zangu nimeziweka pembeni,”amesema Hidaya

Mwigizaji Hidaya Njaidi akiwa na mwanae Othman Njaidi

Amesema akipata nafasi ya kufanya kazi huwa anaitumia vizuri bila kupoteza muda.

“Kilichonisukuma kutimiza ndoto ya uigizaji ni hisia ya kujitolea. Sijui nina nini kila nitakapoonekana tangu utotoni, jina langu lilikuwa likitajwa kila sehemu. Iwe kwenye maombi, kuimba, kucheza, au hata kubeba adhabu darasani ili wenzangu wasamehewe.

“Mara nyingi mwalimu alikuwa anatusamehe wote, hivyo nilikuwa na bahati ya kutangulizwa. Nikipata nafasi, huwa sifanyi makosa hata kidogo. Nilipojaribu mara ya kwanza, nikaishi na ndoto yangu na hatimaye ikatimia. 

“Niliwahi kutamani kuonekana kwenye runinga kupitia kuhojiwa au vipindi mbalimbali. Nilipopata nafasi ya kuigiza, nilishikilia kikamilifu,” amesema Hidaya

Mwigizaji Othman Njaidi ambaye ni mtoto wa Hidaya Njaidi

Aidha, mwanamama huyo ametoa ushauri kwa wanawake na mabinti ambao wanatamani kufuata nyayo zake. Akiwashauri kujipima kwanza kabla ya kuingia katika uigizaji.

“Wanaotamani kwanza wajipime, wanataka kweli kuwa waigizaji au wanataka iwe njia ya kufanya mambo mengine. Kama biashara, uongozi, au kujulikana?. Niwaambie tu aanaa haina mwenyewe na badala yake inahitaji juhudi, heshima, nidhamu, na kwenda sambamba na muda,”amesema

Amesema mbali na uigizaji ni Mwenyekiti wa Jukwaa la Kumuwezesha Mwanamke Wilaya ya Ubungo.

“Jukwaa lina  kata 14 mitaa 90 wajasiliamali wanawake wote ni watu wangu nawaongoza. Lakini pia mimi ni Makamu Mwenyekiti Jukwaa Mkoa wa Dar es Salaam tena wa kupigiwa kura,”amesema

Alisema wanawake wakache kazi bila kuyumbishwa na jambo lolote.

“Tutunze familia, tulinde familia upande wa malezi na maadili.   Mwanamke kamata fursa uchakarike kama ambavyo Mama Samia anavyotuonesha nuru kupitia kazi zake,”amesema.

Ikumbikwe Hidaja ni mama mzazi wa mwigizaji Othman Njaidi, kijana aliyejizolea umaarufu kupitia Marehemu Kanumba ambaye ndiye alikuwa mtu wa kwanza kufanya naye kazi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *