
Moshi. Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba amewataka wananchi wa Jimbo la Vunjo, mkoani Kilimanjaro kuacha mazoea ya kubadilisha wabunge kila baada ya miaka mitano, akisema tabia hiyo inachangia kuchelewesha kukamilika kwa miradi waliyoianzisha.
Dk Mwigulu ameyasema hayo leo Februari 20, 2026 wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara k eneo la Chekereni, Jimbo la Vunjo, Wilaya ya Moshi mkoani hapa wakati akijibu hoja ya Mbunge wa Jimbo hilo, Enock Koola aliyoeleza mbele ya Waziri huyo kwamba ni kama Jimbo hilo limesahaulika.
“Mmemsikia Mbunge amesema Vunjo imesahaulika, na kwa kweli ukiangalia hoja zilizoletwa ni nyingi mno, zinatoa ushahidi kwamba Vunjo imesahaulika,”
Amesema “Sasa niwaambie siri moja, niseme nisiseme?Vunjo mnasahaulika kwasababu mnabadili mno viongozi, kila miaka mitano anaondoka, yaani pale Iramba sisi tukiwa na mbunge mmoja ‘mimi’ hapa nyie mshabadili wabunge watano.
Aidha, amewataka wananchi hao kuendelea kumuamini mbunge Koola kwa kuwa bado ni kijana na anaweza kupambania maendeleo ya wanavunjo.
“Mtu akishaandaa notisi vizuri na akishaanza kufuatilia mnamwondoa na notisi zake, sasa sasahivi mmeleta Mbunge kijana kabisa na hapa aliniona Dodoma akanielezea mambo ya Vunjo kama vile haitoshi juzi akananiona na jana kuaniona na nimekaa naye lisaa limoja kuandika, nimemaliza kuandika na leo amekuja tena hapa kusema,” amesema Dk Mwigulu.
Amesema “Mwachieni huyu ashughulike na hizi hoja, maana kutafuta mbunge mwingine ataanza kupambana kulinda ubunge na kuacha hoja.Mmenihakikishia hamtafuti Mbunge mwingine, kwa hiyo tuhangaike na maji, barabara, vituo vya afya, soko na Halmashauri, na madai si ndio?.”
Awali akiwasilisha changamoto za Jimbo hilo, mbunge Koola amesema Jimbo hilo linachangamoto mbalimbali ikiwemo suala la afya, maji pamoja na changamoto ya barabara.
“Jimbo la Vunjo sisi ni watu wa shukran sana ndani ya miaka mitano ya Rais Samia Suluhu Hassan ametuletea zaidi ya Sh60 bilioni kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli za maendeleo, pamoja na hayo zipo changamoto mbalimbali lakini mheshimiwa Waziri Mkuu jimbo letu la Vunjo kwa muda mrefu sana limesahaulika kutokana na changamoto mbalimbali,”amesema Koola.