
Arusha. Serikali kupitia mpango mkakati wa kupambana na ukatili wa kijinsia dhidi ya watoto na wanawake imefanikiwa kuanzisha madawati 115 ya kupinga ukatili katika masoko mbalimbali kwenye mikoa 12 na halmashauri 88 hapa nchini.
Hayo yalisemwa leo Ijumaa, Februari 20, 2026 jijini Arusha na Mkuu wa Idara ya Usimamizi wa Elimu Ofisi ya Waziri Mkuu, Dk Teresia Kilite wakati akifungua kikao kilichojadili mazingira salama maeneo ya umma.
Dk Teresia amesema Serikali imefanikiwa kuweka mabango 8,015 yanayopinga ukatili katika maeneo mbalimbali ya serikali za mitaa pamoja na kufanya midahalo 4,748 kuhusu sababu za ukatili na mbinu za kuzuia ukatili huo katika jamii.
Aidha alisema wamefanikisha kufanyika kwa mikutano 61,387 ya kujadili masuala ya ukatili katika vijiji 29 kati ya vijiji 12,319 sawa na asilimia 0.24 ambapo ambavyo vimetunga sheria ndogo za kupinga vitendo vya ukatili.
Vilevile wameanzisha madawati ya Ustawi wa Jamii katika vituo vya mabasi kwa lengo la kuasaidia waathirika na kuazuia usafirishaji haramu na vitendo vya ukatili.
“Licha ya kuzungumzia mafanikio hayo bado Serikali ina kazi kubwa ya kufanya, hususani katika kuongeza kasi ya utungaji wa sheria ndogo katika vijiji vyote na kuimarisha uratibu na ufuatiliaji wa utekelezaji,” amesema Dk Teresia.
Kwa upande wake, Ofisa Miradi wa Shirika la Kimataifa la Wanawake (UN WOMEN), Lucy Tesha amesema shirika hilo limekuwa miongoni mwa wadau wanaofanya kazi na Serikali ya Tanzania katika kutekeleza mpango kazi wa kitaifa wa kutokomeza ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto.
Ofisa Miradi huyo anayehisika na Masuala ya Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto, amesema mbali ya mpango kazi wa kitaifa wa kutokomeza ukatili wa kijinsia pia wamekuwa wakihamasisha usawa wa kijinsia.
“Ushiriki wetu katika kikao kazi hiki ni kuunga mkono mipango ya Serikali ili kuhakikisha utekelezaji wa mpango kazi wa kitaifa unakwenda vizuri hasa tukijikita zaidi kwenye suala la mazingira salama katika maeneo ya jumuiya,” amesema Lucy
Pia amesema kwa mujibu wa takwimu za kidunia na za kitaifa tatizo la ukatili wa kijinsia bado liko, hivyo imesababisha Serikali kuweka nguvu katika mapambano na udhibiti wa vitendo vya ukatili ikiwamo kutunga sera na sheria nzuri za kuzuia matukio hayo.