Njombe. Mbunge wa Viti Maalumu (Chaumma) Mkoa wa Njombe, Sigrada Mligo amehoji kusuasua kwa ujenzi wa Barabara ya Itoni – Lusitu kuelekea wilayani Ludewa ili kuwaondolea adha wananchi wanaotumia barabara hiyo kwa shughuli za kiuchumi na kijamii.

Kipande cha barabara ya Itoni – Lusitu, chenye urefu wa kilomita 50, kinaunganisha wilaya mbili za Njombe na Ludewa, ujenzi wake unasuasua ambapo mpaka sasa hakijakamilika licha ya ahadi za kukamilisha ujenzi wa barabara hiyo kutolewa mara kadhaa.

Sigrada amehoji kuhusu jambo hilo leo Februari 20, 2026 wakati wa kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Njombe (RCC) kilichofanyika Ofisi za Mkuu wa Mkoa.

Amesema kwa mujibu wa mkataba wa ujenzi wa barabara hiyo, ilitakiwa kukamilika mwaka 2024 na baadaye mkandarasi kuongezewa muda mpaka Machi 2026, lakini mpaka sasa hakuna kinachoendelea.

Amesema ni miaka minne sasa tangu kuanza kwa ujenzi huo lakini anashangaa kuona mhandisi mshauri wa mradi anaishi kwenye nyumba ya kulala wageni kinyume na utaratibu na kwamba anaiongezea mzigo Serikali.

“Kwenye hii barabara nashangaa kuona mhandisi mshauri, kwa taarifa nilizonazo, nyumba yake haijaisha mpaka leo na anaishi gesti,” amesema Sigrada.

Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Ruth Shalua amesema tayari wameshatoa maelekezo kwa mhandisi mshauri kulipia samani ambazo alikuwa bado hajalipia ili kuweza kuishi eneo la mradi.

“Kuhusu mhandisi mshauri kukaa nyumba ya wageni, tayari amepewa mwongozo kuhusu samani ambazo alikuwa hajazilipia, sasa anakwenda kuzilipia,” amesema Shalua.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka amesema Serikali itaendelea kujenga miundombinu na hata hivyo amewataka viongozi wa mkoa huo kuendelea kufikiria kwa kina namna ya kuinua uchumi wa wananchi wa Njombe.

“Mwanzo niliwaambia natamani kuona Makambako inakuwa Mkuranga au Kibaha na kuweka maeneo ya biashara ili kuvutia watu wanaokuja mkoani Njombe,” amesema Mtaka.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *