MASHABIKI wa soka nchini wameanza kuhesabu siku kabla ya kushuhudiwa pambano la kwanza la Kariakoo Derby katika Ligi Kuu Bara msimu huu, lakini kuna kibarua kigumu kinawakabili makocha wa Simba na Yanga ambao wanaenda kukutana kwa mara ya kwanza.
Ndiyo, kuna siku kama nane kuanzia leo Jumamosi hadi Machi Mosi itakapopigwa mechi ya Dabi ya Kariakoo ya Ligi Kuu Bara kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, visiwani Zanzibar ikiwa ni mara ya kwanza kwa mechi ya Ligi Kuu ya Dabi ya Kariakoo kupigwa huko.
Lakini wakati pambano hilo likisubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka waliopo ndani na nje ya nchi, Yanga na Simba kila moja itashuka uwanjani mara mbili sawa na dakika 180 katika mechi za viporo zilizokaa kimtego kwa makocha wa timu hizo, Pedro Goncalves na Steve Barker.
Kariakoo Dabi ya mwisho tulishuhudia Yanga chini ya Romain Folz ikiibuka na ushindi wa bao 1-0 katika Ngao ya Jamii iliyochezwa Septemba 16, 2025, wakati huo Simba ilikuwa ikifundishwa na Fadlu Davids.
Makocha wote hao waliokutana katika dabi hiyo ya Ngao ya Jamii hawapo tena na timu hizo zitakutana zikiwa na makocha wapya ambao tayari wameshaonyesha uwezo walionao.
Pedro alitambulishwa Yanga Oktoba 25, 2026 akichukua mikoba ya Folz, anakwenda kucheza Dabi ya kwanza kama ilivyo kwa Barker aliyechukua nafasi ya Dimitar Pantev Desemba 19, 2025 aliyedumu kwa muda mchache mno tangu alipopewa kijiti cha kuliongoza jahazi la Msimbazi kutoka kwa Fadlu akifundisha kwa takribani miezi miwili.
Katika dakika hizo 180, Simba inaonekana kuwa na mtihani mgumu mbele yake kutokana na mechi zote itacheza nje ya Dar es Salaam katika mikoa tofauti, huku Yanga ikicheza ugenini na nyumbani.
MECHI ZENYEWE
Februari 22, 2026, kwa maana ya kesho Jumapili, wakongwe hao kila mmoja atajitupa uwanjani kusaka ushindi. Kila timu itakuwa ni mechi ya tisa katika Ligi Kuu kwa msimu huu.
Simba itaifuata Tanzania Prisons kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, katika mechi ambayo inazikutanisha timu zote zilizotoka kupata ushindi wa michuano ya Kombe la Shirikisho (FA) hatua ya 64 Bora.
Awali Prisons ilitangaza mechi dhidi ya Simba itaicheza Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma, kutokana na dimba lao la nyumbani Sokoine kufungiwa kwa kukosa vigezo vya kikanuni, lakini siku tatu kabla ya mtanange huo kwa maana ya Februari 19, 2026, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuufungulia, hivyo Wajelajela hao watabaki maeneo yao ya kujidai.
Kama mechi hiyo ingebaki jijini Dodoma, ingekuwa nafuu zaidi kwa Simba kwani baada ya kumalizana na maafande hao wa Prisons, Februari 25, 2026 ina kibarua kingine Uwanja wa Jamhuri kukabiliana na Dodoma Jiji, timu ambayo kwa siku za karibuni imekuwa na makali eneo la ushambuliaji likiongozwa na Edgar William mwenye mabao matano.
Kwa upande watetezi wa ligi hiyo, Yanga kesho itaifuata Namungo kwenye Uwanja wa Majaliwa uliopo Rungwa Lindi, kisha Februari 25, 2026 itarejea Dar es Salaam kukabiliana na kinara wa ligi kwa sasa, JKT Tanzania kwenye Uwanja wa KMC Complex, Mwenge.
UZITO WA DAKIKA 180
Dakika hizo 180 sawa na mechi mbili, zimebeba pointi sita zenye maana kubwa sana kwa wakali hao Ligi Kuu Bara.
Ukiangalia msimamo wa sasa ulivyo, tofauti ya pointi kwa timu hizo ni tatu tu, Yanga ikiwa nazo 22, Simba 19, huku zote zikishuka uwanjani mara nane.
Pale juu kuna JKT Tanzania iliyocheza mechi 16 na kuvuna pointi 28 ambazo Yanga kama ikizifunga Namungo na JKT Tanzania, itarejea kileleni.
Kwa Simba, hizi ni mechi za kuirudisha timu katika mapambano ya ubingwa ilioukosa kwa misimu minne mfululizo sasa ukibebwa na Yanga. Tofauti ya pointi tatu kwa sasa, haipaswi kuwa zaidi ya hapo ili kuusogelea ubingwa japo ni mapema kusema hivyo.
Kama Simba itavuna pointi hizo sita, itafikisha 25 na Yanga ikifanya hivyo pia maana yake Kariakoo Dabi atakayeshinda atajiweka pazuri zaidi katika msimamo na huenda mechi hii ikatoa taswira ya timu hizo zinamaliza vipi duru la kwanza kabla ya kuanza hesabu za duru la pili.
WAPINZANI WAO WAPOJE?
JKT Tanzania na Namungo ndio wapinzani wa Yanga kabla ya kufika Dabi ya Kariakoo. Timu hizo zimepishana madaraja kwa sasa. JKT Tanzania imeanza na moto hadi kukaa kileleni ikipishana mara kadhaa na Yanga wakati Namungo ikiwa nafasi ya tano ikikusanya pointi 20 baada ya kucheza mechi 14 dhidi ya Yanga itahitimisha duru la kwanza.
Katika mechi tano za mwisho, Namungo imeshinda moja pekee dhidi ya KMC kwa bao 1-0, huku ikipoteza mbili mfululizo za hivi karibuni na sare zingine mbili zilifuatana ilipotoka kushinda.
Licha ya Namungo kutokuwa na matokeo mazuri mfululizo, lakini ina kinara wa mabao wa ligi ambaye ni Fabrice Ngoy aliyepachika saba. Ndiye tegemeo eneo la ushambuliaji.
Namungo msimu huu hadi sasa haijapoteza nyumbani ilipocheza mechi sita, imeshinda nne na sare mbili, hata hivyo mbele ya Yanga, Wauaji hao wa Kusini hawana ujanja huku mara ya mwisho dimbani hapo wakichapwa 2-0.
Rekodi za jumla zinaonyesha tangu 2020-2021, timu hizo zimekutana mara 13 katika ligi ni 12 na FA moja, huku Yanga ikishinda mechi nane na sare tano. Namungo haijaonja ushindi.
Ukija dhidi ya JKT Tanzania yenye rekodi ya kupoteza mechi mbili pekee msimu huu kati ya 16 ilizocheza na kukaa kileleni, Yanga pia ni wababe wakishinda mechi nane kati ya 11 walizocheza tangu 2018-2019. Sare zikiwa tatu, wakati JKT Tanzania bado haijaonja ushindi mbele ya mabingwa hao watetezi.
Paul Peter na Saleh Karabaka ambao ni vinara wa mabao JKT Tanzania, wanatajwa ndio wanaibeba timu hiyo, hivyo wanaweza kutibua mipango ya Pedro.
Ukija upande wa pili, Tanzania Prisons ni kama inajitafuta bado haijakaa sawa licha ya kutoka kushinda mechi mbili mfululizo hivi karibuni dhidi ya Namungo katika Ligi na Kombe la Shirikisho (FA) mbele ya Moro Kids.
Katika mechi 13 za ligi ilizocheza, imeshinda tatu, sare tatu na imepoteza saba ikikusanya pointi 12 ikiwa nafasi ya 14.
Kabla ya kuifunga Namungo Februari 14, 2026, Prisons mara ya mwisho ilishinda 2-1 dhidi ya Mbeya City, kisha ikacheza mechi tisa ndipo ikapata ushindi mwingine.
Mechi 10 za mwisho baina ya timu hizi, Prisons imeshinda tatu, Simba ikiibuka kidedea mara sita, sare moja.
Dodoma Jiji ambayo itakuwa kama kipimo cha mwisho kwa Wekundu wa Msimbazi kabla ya Kariakoo Dabi, hivi sasa ni ya sita na pointi 20 ikicheza mechi 15.
Mechi tano za karibuni katika ligi ilizocheza Dodoma Jiji, imeshinda tatu, sare moja sawa na iliyopoteza dhidi ya Yanga.
Katika kukutana kwao tangu 2021-2022, Simba imeshinda mechi zote kumi, hakuna sare wala Mnyama kupoteza. Mara ya mwisho iliibuka na ushindi wa mabao 6-0.
Ni wazi makocha wa timu hizo mbili za Yanga na Simba wameshaanza kupitia mafaili ya mechi za mwisho za Dabi ya Kariakoo na kugundua ugumu uliopo mbele yao, lakini wanajua kuvuka salama katika dakika 180 zilizopo mbele yao kwa kila mmoja itawapa ‘code’ wa kutoboa Machi Mosi.
Rekodi zinaonyesha Simba haijapata ushindi wowote mbele ya Yanga katika mechi sita mfululizo zilizopita za Dabi ya Kariakoo kwa mashindano yote na mara ya mwisho katika Ligi Juni 25 mwaka jana ilipasuka mabao 2-0 na kuwapa watani wao ubingwa wa msimu wa nne mfululizo.
Safari hii chini ya Steve Barker, Wekundu hao watatokaje katika pambano hilo la 115 kwa timu hizo kwa Ligi ya Bara tangu mwaka 1965 , mbele ya Yanga ya Pedro litakalopigwa kuanza saa 2:15 usiku? Ni suala la kusubiri kuona, ila Dabi ya Kariakoo haijawahi kuwa nyepesi na huenda kitawaka wakishausoma mchezo.